Viongozi hao wametangaza msimamo huo katika kongamano la "Quds, Mji
Mkuu wa Milele wa Palestina" lililoitishwa na harakati ya Jihadul Islami
katika mji wa Gaza na kutoa wito wa kuwepo umoja wa kitaifa na
ushirikishaji wa kisiasa sambamba na kuundwa jeshi la kitaifa kwa ajili
ya kulinda matukufu ya ardhi ya Palestina.
Aidha wamesisitizia ulazima wa kusimamishwa ushirikiano na uratibu wa
pamoja wa kiusalama uliopo baina ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na
utawala wa Kizayuni.
Mahmoud Az-Zahar, kiongozi mwandamizi wa harakati ya Hamas ameliambia
kongamano hilo kwamba: walowezi wa Kizayuni watahasirika mno kwa
kuivamia ardhi ya Palestina na akasisitiza kwamba: Wapalestina
hawatoyauza katu matukufu yao kwa ajili ya kupatiwa pesa.
Sheikh Nafidh Azzam, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya
Jihadul Islami, amesema: uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani wa
kuitambua rasmi Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni ni
sawa na kukiuka sheria za kimataifa na akasisitiza kwamba Marekani
inafanya kila njia kulinda usalama wa Israel; nao Wapalestina wanazitaka
nchi za Kiarabu ziangalie upya uhusiano wao na Marekani.
Kasisi Manuel Musallam, kiongozi wa kiroho wa Wakristo wa Palestina
na mjumbe wa Kamati ya Kiislamu na Kikristo ya Kuyahami Matukufu ya
Palestina amewataka walimwengu wasikubali eneo la Mashariki ya Kati
lisukumwe kwenye vita vya kidini.
Amesisitiza kuwa heshima na izza ya
Waislamu na Waarabu imefungamana na Quds na kwamba kukaliwa kwa mabavu
Quds kutawafanya Waarabu wawe duni na dhalili.
chanzo: parstoday.
Comments