Uhusiano wa pande hizo mbili zenye nafasi muhimu katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ulizorota na kuyumba katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.
Mwaka 2011 Uturuki ilikuwa miongoni mwa nchi zilizounga mkono mabadiliko ya utawala nchini Misri. Uungaji mkono huo ulitokana na mfungamano uliokuwepo baina ya Ankara na harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri.
Uturuki iliunga mkono kuchukua madaraka harakati hiyo nchini Misri mwaka 2012 na kulitambua tukio la kuondolewa madarakani serikali ya Muhammad Mursi mwaka mmoja baadaye kuwa ni mapinduzi ya kijeshi.
Kwa msingi huo uhusiano uliokuwa umestawi sana baina ya Uturuki na Misri katika kipindi cha utawala wa Mursi na Ikhwanul Muslimin uliporomoka na kushuka msimu wa kiangazi wa mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani Muhammad Mursi na matamshi yaliyotolewa na Rais wa sasa wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan kuhusu tukio hilo.
Hivyo basi, matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri, Samih Shukri kuhusu suala la kuhuishwa uhusiano wa pande hizo mbili lakini kwa masharti yalilenga siasa za Ankara za kuliunga mkono kundi la Ikhwanul Muslimin.
Hapa linajitokeza swali kwamba, ni nini sababu ya kujitokeza ishara za kutaka kuhusishwa tena uhusiano wa Cairo na Ankara? 
Inaonekana kuwa, suala hilo lina mfungamano na uamuzi uliochukuliwa na Rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu Quds tukufu (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Kutokana na kuwa na viti katika taasisi za kimataifa, Uturuki na Misri zilifanya jitihada zinazofanana za kulaani uamuzi wa Trump wa kuitambua Quds kuwa eti ni mji mkuu wa Israel na kutoa amri ya kuanza mchakato wa kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Baitul Muqaddas.
Misri ni miongoni mwa wanachama wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Nafasi hiyo imeiwezesha Cairo kuwasilisha pendekezo la kuunga mkono Palestina katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kulaani uamuzi wa Donald Trump kuhusu mji wa Baitul Muqaddas.
Pendekezo hilo lilipasishwa na nchi 14 kati ya 15 wanachama wa Baraza la Usalama licha ya kuzuiwa kwa kura ya veto ya Marekani.
Uturuki kwa upande wake ni Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Hivyo, baada ya Marekani kupiga kura ya veto dhidi ya muswada wa Misri katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Uturuki kama mwenyekiti wa OIC ilipendekeza muswada mwingine katika Baraza Kuu la Umoja huo uliolaani hatua ya Donald Trump ya kutangaza mji wa Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa Israel. Azimio hilo lilipasishwa kwa kura 128 za wanachama wa Umoja wa Mataifa. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, harakati ya sasa ya kutaka kuboreshwa tena uhusiano wa Cairo na Ankara ni miongoni mwa matunda ya makosa ya kistratijia Trump kuhusu Quds tukufu.
Suala jingine tunalopasa kuashiria hapa ni kuwa, Ulimwengu wa Kiislamu una haja ya kuimarishwa uhusiano baina ya nchi kubwa na muhimu kama uhusiano baina ya Uturuki na Misri na uhusiano baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Misri.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kutupilia mbali hitilafu na mifarakano baina ya madola makubwa ya Waislamu na kuwa na msimamo mmoja kuhusu masuala yanayohusiana na Umma kunaweza kuimarisha msimamo wa Ulimwengu wa Kiislamu katika mfumo wa kimataifa na kuzuia maamuzi yasiyo ya kuwajibika na ya kidhalimu ya tawala za Kimagharibi. 
chanzo:parstoday.
Comments