Mahakama
Kuu imetupa maombi ya Swabaha Mohamed aliyeangua kilio mbele ya Rais
John Magufuli akidai kudhulumiwa mirathi ya mumewe, baada ya
kujiridhisha kuwa sababu alizotoa hazikuwa na ukweli.
Katika maombi hayo, Swabaha alitaka ateuliwe kuwa msimamizi wa mirathi.
Mama
huyo anayedai ni mjane wa Mohamed Shosi Yusufu wa mkoani Tanga alikuwa
akiomba kuongezewa muda wa kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya
Wilaya Tanga.
Mahakama
ya Wilaya Tanga ilitupilia mbali rufaa yake ya kupinga uamuzi wa
Mahakama ya Mwanzo Tanga kumteua Saburia Shosi ambaye ni mtoto wa
marehemu kuwa msimamizi wa mirathi hiyo badala yake.
Mahakama
Kuu katika uamuzi uliotolewa Jumatano na Jaji Amour Khamis, imeyatupa
maombi hayo baada ya kuridhika kuwa sababu zake za kuomba kuongezewa
muda si za kweli.
Katika
uamuzi huo, Jaji Khamis alikubali hoja za Saburia kupitia kwa wakili
wake, Abdon Rwegasira kuwa mwombaji (Swabaha) hakutoa sababu za msingi
za kustahili kuongezewa muda wa kukata rufaa na kwamba sababu ya ugonjwa
na kulazwa aliyoitoa si ya kweli.
Hii ni mara ya pili kwa Swabaha kufungua maombi mahakamani hapo akiomba kuongezewa muda wa kukata rufaa.
Ombi la awali lilitupwa kutokana na kutokuwa na sababu za msingi kisheria za kuchelewa kukata rufaa.
Awali,
alifungua maombi mwaka 2016 akidai alichelewa kupata nakala ya mwenendo
wa kesi na hukumu aliyokuwa anataka kuikatia rufaa.
Oktoba 2016 Mahakama Kuu katika uamuzi uliotolewa na Jaji Khamis iliyatupilia mbali maombi hayo.
Mapema
mwaka huu alifungua tena maombi hayo mahakamani hapo na akatoa sababu
nyingine, akidai alichelewa kukata rufaa kwa kuwa alikuwa amelazwa
hospitalini kutokana na kuwa mgonjwa.
Aliwasilisha
mahakamani kadi ya kuruhusiwa kutoka Tanga Central Health Centre,
ikionyesha alilazwa Oktoba 9, 2016 na akaruhusiwa Oktoba 16, 2016.
Wakili
Rwegasira aliwasilisha mahakamani barua na kiapo cha mkurugenzi wa
kituo hicho aliyejitambulisha kuwa ni Dk H. I. Ngayomela, akikana mama
huyo kulazwa hospitalini kwake.
Dk
Ngayomela alisema ingawa kadi inaonekana ni ya hospitali yake, lakini
hajui aliipataje, huku akisema tarehe ya kulazwa na kuruhusiwa pamoja na
namba ya jalada vinavyoonekana katika kadi hiyo ni vya mgonjwa mwingine
tena wa kiume.
Alisema mwandiko kwenye kadi haufanani na wa daktari yeyote kituoni kwake, huku akidai haina saini.
Siku
chache baadaye, Swabaha aliwasilisha maelezo mengine mahakamani ambayo
hata hivyo, yalikuwa yameandikwa kwenye karatasi bila kubainisha kuwa
imeandikwa kwa nani, akidai inatoka kwa Dk Ngayomela akikiri kumtambua
na kwamba kuna makosa yalifanyika wagonjwa wawili wakapewa namba moja ya
jalada.
Maelezo
hayo yalisababisha wakili Rwegasira aiombe Mahakama mama huyo afike
mahakamani kuhojiwa kuhusu mkanganyiko huo na alishindwa kutoa maelezo
ya kuiridhisha Mahakama.
Jaji
Khamis katika uamuzi wake alisema amebaini kuwa kuna ufa wa wazi katika
madai ya mama huyo ya kuugua na kulazwa, kutokana na kushindwa kutaja
hata jina la daktari au muuguzi aliyemhudumia kwa siku saba.
Alisema
hata barua ya pili ya Dk Ngayomela inayoeleza kumtambua haiwezi
kufafanua na kuondoa shaka ya tuhuma alizotoa mwanzoni kwenye kiapo cha
upande wa mjibu maombi.
Jaji
Khamis alisema Swabaha katika mahojiano mahakamani hakuweza kufafanua
utata huo na kwamba, majibu yake wakati wa madodoso, akihojiwa na wakili
Rwegasira yalikuwa ni ya kujikanganya.
“Mwombaji
alishindwa hata kutaja majina ya madaktari na wauguzi waliokuwa
wakimhudumia kwa muda wa siku saba alizodai alilazwa hospitalini hapo.
Alimtaja Dk Ngayomela tu kama anayeweza kumkumbuka katika orodha ya
madaktari waliomhudumia katika ugonjwa wake,” alisema.
Jaji
Khamis alisema, “Kwangu hili haliwezi kuwa kweli kwa sababu kama
angekuwa amemhudumia kama alivyodai asingeweza (Dk Ngayomela) kushindwa
kutambua mwandiko wake katika kadi ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, kwa
kiwango cha kukana uhalali wake kwa kiapo.”
Alisema maombi hayo hayana mashiko hivyo kuyafuta na kuamuru Swabaha kulipa gharama za uendeshaji wa shauri hilo.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments