Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka jana ulibaini zaidi ya watu milioni moja duniani huambukizwa maradhi ya zinaa kwa siku na kila mwaka takriban watu milioni 357 huambukizwa kati ya kaswende, kisonono, klamidia au trikmonasi.
Utafiti wa mwaka 2012, WHO inathibitisha zaidi ya wajawazito 900,000 waliambukizwa kaswende iliyowasababishia madhara katika ujauzito ikiwamoa kujifungua watoto wafu.
Hata hivyo, inaelezwa kati ya maradhi manane ya zinaa, manne yanatibika, nayo ni kaswende, kisonono, chlamydia na tichomoniasis.
Mengine manne yanasababishwa na virusi na hayana tiba ambayo ni hepatitis B, HIV, Herpes Simplex Virus na Human Papilloma Virus HPV.
Maradhi haya huambukizwa hasa kwa njia ya ngono zembe na madhara makubwa kwa mjamzito.
Madhara ya kaswende kwa mama na mtoto wakati wa ujauzito.
Ugonjwa huu ni tishio na husababishwa na bakteria anayeitwa treponema pallidum.
Kaswende wakati wa ujauzito inaweza kuwa hatari kubwa kwa kiumbe kilichopo tumboni kwa kukifanya kutoumbika vizuri (deformity) na kifo.
Wajawazito wengi walio katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania huchunguzwa kama wanamaambukizi ya ya ugonjwa huo katika juma ya kwanza ya mimba.
Lengo la kufanya hivito anamaambukizi hayo, aweze kutibiwa kabla mtoto hajaathirika.
Kisonono
Kisonono au kwa jina linguine unafahamika kisalisali ni miongoni mwa maradhi ya zinaa yanayosababisha bakteria wafahamikao kisayansi Neisseria gonorrhoeae. Bakteria hawa hushambulia utandotelezi unaozunguka sehemu za siri.
Kwa wanawake, maambuki hutokea katika urethra, sehemu za siri au mlango wa uzazi (cervix).
Ingawa muwasho unaotokana na majimaji katika sehemu za unaweza kuwa mkubwa, mara nyingi dalili hizi huwa ni chache au hazitokei kabisa katika hatua za awali.
Kisonono isiyotibiwa inaweza kusababisha PID (Pelvic Infiammatory disease) kwa wanawake. Watoto wanaozaliwa na mama wenye kisonono huwa na hatari ya kuambukizwa wakati wa kuzaliwa; maambukizo haya yanaweza kusababisha maradhi ya meno kwa wachanga.
Klamidia
Klamidia ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na bakteria zinazoitwa kisayansi Chlamydia trachomati. Ugonjwa huo huwa hauonyeshi dalili za wazi kwa karibia asilimia 75.
Hivyo, wanawake wengi wenye maambukizi hushindwa kubaini mapema. Wakati dalili zinapoanza kujitokeza, kwa upande wa wanawake huanza kutokwa damu nje ya kipindi chao cha hedhi, maumivu wakati wa kukojoa, kutokwa usaha sehemu za siri, au maumivu chini ya kitovu.
Kama utaachwa bila kutibiwa hususan kwa wanawake, klamidia inaweza kuleta madhara makubwa.
Kwani huharibu tishu za uzazi za mwanamke na kusababisha uvimbe katika fupanyonga (pelvic inflammatory disease, PID).
PID inaweza kusababisha mauvimu makali katika fupanyonga, utasa au ugumba au utata katika ujauzito ambao unaweza kusababisha kifo.
Watoto waliozaliwa na mama aliyeambukizwa klamidia huwa na hatari ya kupata upofu au maambukizi katika mapafu.
Trikomonasi
Trikomonasi husababishwa na maambukizi ya protozoa anayefahamika kisayansi Trichomonas vaginalis. Ugonjwa huu husababisha muwasho na karaha katika uke kwa wanawake. Kwa mama mjamzito inaweza kumsababishia akajifunhua kabla ya muda, kujifungua njiti na maambukizi kwa mtoto baada ya kujifungua.
Ukimwi
Ukimwi ambao ni ukosefu wa kinga mwilini, ni matokeo ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) - Human immunodeficiency virus (HIV).
Ukimwi ni ugonjwa wa zinaa hatari na usiotibika ambao hushambulia mfumo wa kinga ya mwili na kumwacha mgonjwa akiwa hana hata uwezo wa kujikinga dhidi ya maambukizi madogo.
Wakati VVU wanaweza kuenezwa kwa njia nyingine, kujamiiana ndiyo njia hasa ya maambukizi ya virusi hivi.
Wanawake ambao wameathirika na virusi vya ukimwi wanaweza kumwambukiza mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua, au mara kadhaa wakati wa kuwanyonyesha. Bila matumizi ya dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi ni kwa asilimia 15 hadi 30 mtoto anawezaliwa akiwa na maambukizi ya VVU, asilimia 5 hadi 20 kupata maambukizi wakati wa kunyonyeshwa.
Maradhi mengine ni yale yanayosababishwa na Virusi kama Human Papilloma Virus ambayo huweza kusababisha saratani ya shingo ya uzazi, maradhi katika mfumo wa hewa wa mtoto, pia matatizo wakati wa kujifungua.
Hepatitis B, huambukizwa kwa njia ya ngono zembe na maambukizi kwa mtoto wakati wa kujifungua, mtoto anapozaliwa ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa anaweza kuwa na asilimia 90 ya kupona kama endapo alizaliwa nao.
Herpes huambukizwa kwa wakati wa ujauzito na inaweza poromosha ujauzito katika miezi mitatu ya mwanzo cha ujauzito.
chanzo:Mwananchi.
Comments