CUF moto wawaka uchaguzi wa ubunge katika majimbo matatu.

cufChama cha Wananchi (CUF) kimezidi kupata athari kutokana na mgogoro wa uongozi unaokikabili baada ya upande wa Profesa Ibrahim Lipumba kupitisha wagombea ubunge katika majimbo matatu.

Hatua hiyo imepingwa na upande wa Katibu Mkuu wa chama hicho Seif Sharrif Hamad kwa maelezo kuwa chama hicho kwa kushirikiana na vyama vingine vinavyounda Ukawa vimeshatoa msimamo wa kutoshiriki. Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), uchaguzi katika majimbo hayo ya Singida Kaskazini, Longido na Songea Mjini utafanyika Januari 13, 2018.

CUF upande wa Profesa Lipumba kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya ulisema umewapitisha Delfina Mlelwa kugombea Singida Kaskazini, Japhary Mneke (Songea Mjini) na Kisiongo Mayasek Olukuya (Longido).

Naibu Mkurugenzi wa Uchaguzi upande wa Maalim Seif, Shaweji Mketo alisema hawawatambui wagombea hao walioteuliwa na kupitishwa na NEC. “Wagombea hawa hawajapitishwa wala kuidhinishwa rasmi na vyombo vyenye mamlaka ya uteuzi ndani ya CUF na hatutashiriki uchaguzi huu wa marudio,” alisema.

Alisema sababu ya kutoshiriki uchaguzi huo ni kuheshimu na kusimamia msimamo wa pamoja wa vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, NLD na chama mwalikwa Chaumma, uliotolewa baada ya kuibuka changamoto katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata 43.

Katika tamko lao la pamoja lililosoma na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, vyama hivyo vilisema kutokana kasoro za uchaguzi huo, NEC na Serikali walipaswa kukaa mezani kujadiliana na kusitisha uchaguzi huo ili wadau wakutane kufanya tahmini ya changamoto zilizojitokeza.

Siku tatu zilizopita, Chadema ilikumbana na changamoto inayofanana na hiyo, lakini ilitokana na mgombea wake kujitosa kuwania ubunge Singida Kaskazini bila kupitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho, hivyo kulazimika kujitoa.

chanzo: zanzibar24.

Comments