
Katika mkutano huo ulioongozwa na Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango wafanyabiashara kutoka kampuni mbalimbali za
binafsi walieleza changamoto wanazokumbana nazo na kushauri njia
muafaka za kuondokana na changamoto hizo ili kuweka mazingira mazuri ya
biashara nchini.
“Lengo letu la msingi kuwepo katika mkutano huu ni kutaka
kuhakikisha sekta binafsi zinakuwa karibu na serikali ili kupatikane
nafasi ya kuelezana yale yanayoonekana ni kikwazo katika uwekezaji, kama
inavyofahamika kazi ya benki ni kutoa mikopo na kuwezesha kampuni
kutimiza malengo yake na kumudu kulipa kodi,” alisema Bw Godwin Seiya.
Akizungumzia hali halisi ya kiuchumi nchini Bw Seiya
alisema kodi ndiyo inayoendesha nchi hivyo hakuna namna ambayo serikali
itaruhusu ukwepaji kodi lakini mbali ya hayo serikali imefungua milango
ya majadiliano na kuwasikiliza wafanyabiashara mambo yanayowakwaza.
“Hii ni heshima kubwa tumepewa wafanyabiashara, katika
mkutano huu kama alivyoeleza Waziri Mpango, ndipo ambapo sehemu ya
bajeti ya mwaka ujao wa fedha itatengenezwa kupitia mawazo yaliyotolewa
na wajumbe,” alisema mhudhuriaji mmoja.
Akihutubia wajumbe katika mkutano huo wa siku moja, Waziri
Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi na mwenyekiti alisema serikali haina
tatizo na kubadili mfumo wa kodi kwa sababu kila siku wanatafuta namna
nzuri ya kukusanya kodi bila kuwakwaza wafanyabiashara.
“Naomba niwaeleze kuwa hata serikali inafurahi kuwa na
mikutano ya namna hii, kwa sababu tunatarajia tutapata mapendekezo
yanayotekelezeka. Katika mazingira haya niliyoeleza ningependa kuona
tunapata mfumo wa kodi utakaofungulia nguvu ya sekta binfsi,” alisema
Dkt. Mpango.
Alisisitiza kuwa kwa sasa Tanzania ni miongoni mwa mataifa
yanayoendelea ambayo yanajipanga kuwa na uchumi wa kati kwa kutegemea
mapato ya ndani kwa sababu wahisani wamepunguza kutoa misaada na mikopo.
“Tukiamua kufanya kazi pamoja na kuweka nguvu zetu kwa
kusikilizana changamoto na kupata majibu mazuri; hakuna
kitakachotushinda. Katika hotuba ya bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/18
tuliingiza mambo mengi kutokana na ushauri wa sekta binafsi.
Tutaendelea kufanya hivyo na hii ni ahadi ya serikali,” alisema Dkt.
Mpango.
Kwa upande wake mwakilishi wa jumuiya ya wenye viwanda
nchini (CTI) Dk. Samwel Nyantahe pamoja na mambo mengine, amesisitiza
umuhimu wa serikali pamoja na jumuiya ya wafanyabiashara kuendelea
kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika
sekta binafsi.
“Sekta binafsi ina changamoto nyingi tunazokabiliana nazo,
tutumie vizuri fursa kama hizi za kukutana na serikali kueleza mambo
yanayotukwaza ili yapatiwe majibu, lakini pia kama tuna ya kushauri huu
ndio wakati wake,” alisema Dkt. Nyantahe.
Azania Bank Limited imeweka wazi kuwa ushiriki wake katika
maandalizi ya mkutano huo muhimu kwa sekta binafsi na sekta ya umma ni
kutaka kuwezesha uchumi wa viwanda kwa kuongeza fursa kwa sekta binafsi
ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia ukuzaji uchumi kupitia ulipaji kodi.
chanzo: zanzibar24.
Comments