Wakazi 1,172 wamenufaika na mafunzo ya upanuzi wa makazi ya rais.



Rais John Magufuli
Jumla ya wakazi 1,172 wanaoishi katika vijiji vitano vilivyopo jirani na Ikulu Chamwino mkoani hapa wamenufaika na mafunzo ya kuwaongezea ujuzi ili  washiriki vyema katika upanuzi wa makazi ya Rais.
Neema hiyo imefuatia utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Julai mwaka jana mjini hapa la Serikali kuhamia mkoani hapa kabla ya awamu ya kwanza ya uongozi wake kukamilika.
Tayari Waziri Mkuu, mawaziri, manaibu, makatibu wakuu, manaibu makatibu wakuu na baadhi ya watumishi wameshahamia mjini hapa ikiwa ni utekelezaji wa agizo hilo.

Akizungumza katika mahafali ya tisa ya Chuo cha Veta mkoani hapa, Mkuu wa chuo hicho Ramadhan Mataka amesema  kuwa mafunzo hayo yaliendeshwa chini ya mfumo wa Competent Based Education and Training (CBET).
“Tumeshirikiana na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao tumeshirikiana nao katika kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa baadhi ya washiriki 1,172 kutoka katika vijiji vitano kwa lengo la kuwaongezea ujuzi ili washiriki vyema katika upanuzi wa Ikulu ya Chamwino,” amesema Mataka.
Mataka amesema  pia chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Kazi Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu wamewatambua wanagenzi 260 ambao kati ya hao 241 wamefaulu baada ya kupimwa mkoani Dodoma.
Akizungumzia kuhusu programu hiyo ya wanagenzi, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana Antony Mavunde amesema  chini ya programu hiyo wanawachukua wakufunzi wa Veta na kwenda nao mtaani kwa ajili ya kubaini mapungufu waliyonayo vijana na kuyaziba.
“Baadaye vijana hao tunawapa vyeti vya Veta bila kusoma Veta. Hawa ni vijana 3,900 ambao wako mitaani,”amesema
chanzo:Mwananchi.

Comments