Taasisi iliyotangaza kutoka mikopo kwa wanafunzi yachunguzwa.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepokea taarifa ya kuwepo kwa Taasisi ya Msaada wa kijamii Tanzania (Tanzania Social Support Foundation - TSSF) ambayo inajitangaza kuhusika na kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Katika Gazeti la Mwananchi Toleo Namba 6306 la Novemba 2, 2017 katika ukurasa wake wa Pili iliandika habari iliyosomeka: “Taasisi Yasisitiza Neema Mikopo Elimu ya Juu.” Habari hiyo pia inaelezea juu ya kuwepo kwa mkutano Novemba 30, 2017 kati ya TSSF na Wakuu wa Taasisi za Elimu ya Juu.

Wizara inapenda kuutangazia Umma kuwa Taarifa hizo siyo za kweli kwani TSSF haitambuliwi na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na tayari Wizara imeanza kufuatilia kujua uhalali wa usajili wake, hivyo wananchi hawana sababu ya kuamini kinachotangazwa na Taasisi hiyo.

Wizara inaziomba Taasisi nyingine za Serikali hasa zinazosajili Taasisi za Kiraia kufanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha na usajili wake.

Wakati huohuo, Wizara inamwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo ya TSSF, Bw. Donati Salla, au mwakilishi wake kufika Makao Makuu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, akiwa na nyaraka zote muhimu za utambulisho wa Taasisi yake. Akifika aonane na Katibu Mkuu wa Wizara.

Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA.

chanzo:Mpekuziblog.

Comments