Serikali yaipongeza ATI kwa mkutano wa Afrika.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu KijajiSERIKALI imeupongeza Umoja wa Kampuni za Bima Tanzania (ATI) kwa kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa sekta ya bima barani Afrika, hivyo kuitangaza Tanzania kimataifa.
Mkutano huo wa Taasisi ya Bima Afrika (AIO) una kaulimbiu isemayo Kuelekea Uchumi wa Viwanda, Majukumu ya Bima ya Maisha katika kufanikisha Maendeleo Endelevu kwa Afrika.

Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji (pichani) ambaye alimwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema ATI imeonesha namna inavyoitangaza nchi na kukuza uchumi wake. Mkutano huo wa siku tatu unaofanyika Arusha, unahudhuriwa na wadau wa Bima kutoka Afrika na nje ya Afrika.
Unatarajiwa kufikia tamati leo. Waziri huyo alizipongeza kampuni za bima kwa kazi nzuri zinayofanya, huduma na bidhaa zao. Amezitaka kuwafikia Watanzania wengi zaidi vijijini ili kusaidia kukuza uchumi na kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba kwa wananchi.
Amezipongeza taasisi hizo za bima kuja na kaulimbiu inayoshabihiana na ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, ajenda ya serikali sasa. Alizitaka pia kampuni za bima kutumia fursa ya miradi mikubwa mikubwa Tanzania ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga na mingine ya ujenzi wa barabara za juu katika kufanya biashara na kukuza uchumi.
Naibu Waziri alizitaka kampuni za bima nchini kuajiri vijana wa Kitanzania wanaomaliza vyuo vikuu badala ya kuchuma na kupeleka fedha nje. Mwenyekiti wa ATI, Sam Kamanga aliahidi watazingatia ushauri wote alioutoa Waziri.
chanzo:Habarileo.

Comments