Majibu ya waziri mkuu wa Canada sakata la ndege ya Tanzania (Bombardier).

Image result for tz aire
Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amesema hawezi kuingilia uhuru wa mahakama ambayo anaamini itatenda haki kuhusu sakata la ndege ya Tanzania (Bombardier) ambayo inashikiliwa nchini humo.

Kauli hiyo ya Waziri Mkuu wa Canada imekuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Magufuli aliposema kuwa, amemwandikia barua kiongozi huyo ili kujua hatma ya ndege hiyo.

Rais Magufuli alizungumza hayo Novemba 6 wakati wa uzinduzi wa uwanja wa ndege mjini Bukoba na kueleza kuwa ametuma pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kwenda nchini Canada kushughulikia suala hilo kisheria.
“Nimeshaandika barua kwa Waziri Mkuu wa Canada nikimwambia washughulikie hii, haiwezekani ndege ikakaa kule miezi sita wakati sisi tulitaka iwe inakuja kwenye uwanja wa Bukoba. Nimeshamtuma pia mwanasheria mkuu anapambana nao kwa njia ya kisheria,” alisema Rais Magufuli.
Kupitia taarifa iliyochapishwa katika gazeti la National Post la nchini Canada, Waziri Mkuu wa nchi hiyo amesema kuwa, ni bahati mbaya sakata hilo limechelewesha kuwasili kwa ndege. Lakini serikali ya Canada haipo katika nafasi ya kuweza kuingilia suala hilo. Tuna imani kuwa mahakama itashughulikia suala hili kwa ufanisi mkubwa bila upendeleo.
Ndege hiyo, Bombardier Q400-8 inashikiliwa kwa amri ya mahakama kutokana na shauri lililopo kati ya Serikali na kampuni ya Stirling Civil Engineering ya nchini Uingereza ambayo iliingia mkataba na serikali kuhusu ujenzi wa barabara ya Wazo Hill – Bagamoyo ambapo serikali ilivunja mkataba huo kabla haujakamilika.
Kampuni hiyo ilikwenda katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi na ilishinda kesi na kupewa kibali cha kikamata mali za Tanzania katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji, Uganda na Canada baada ya serikali kutolipa fidia ya fedha iliyokuwa imeamuriwa na mahakama.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano yupo nchini Canada kushughulikia suala hilo.
chanzo:zanzibar24.

Comments