CCM yakemea vitendo vya kuhujumu vinavyofanywa na wasiotaka maendeleo nchini.

Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimekemea vitendo vya kuhujumu miundombinu ya maji safi na salama vinavyofanywa na baadhi ya watu wenye nia ya kukwamisha juhudi za serikali katika kuwapelekea wananchi huduma muhimu za kijamii.

Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi katika ziara Maalum ya kukagua baadhi ya maeneo yaliyohujumiwa miundombibu hiyo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja huko katika shehia ya Mkwajuni katika Kisima namba 4 cha Kiashange  Wilaya ya Kaskazini “A”.

Kisima hicho ambacho kimeibiwa waya za umeme wa mashine inayosukuma maji mpaka katika tangi kubwa la Nungwi linalosambaza maji katika maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Kaskazini “A” na vitongoji jirani hali inayosababisha usumbufu kwa baadhi ya wananchi wa maeneo hayo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitumia fedha nyingi za walipa kodi kuimarisha miundombinu ya maji mijini na vijijini ili wananchi kuondokana na kero ya ukosefu wa huduma hiyo lakini kuna baadhi ya watu kwa maslahi yao binafsi wamekuwa wakiharibu  miundombinu hiyo kwa makusudi .
Dk.Mabodi alieleza kwamba maji ni miongoni mwa nishati muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu hivyo yanapokosekana ama kutopatikana kwa wakati yanasababisha usumbufu na madhara makubwa hasa katika maeneo ya huduma za kijamii yakiwemo katika nyumba za ibada, hospitalini, shuleni na kwa wagonjwa wanaotibiwa wakiwa majumbani mwao.
Alisema  vitendo vya kuziba mipira ya maji kwa kutumia zege, kuiba mipira ya kusambazia maji, mashine, waya za umeme, Transfoma  pamoja  kufunga mifugo katika maeneo ya miundombinu ya maji ni tabia zisizokubalika katika jamii na sheria za nchi.
Naibu Katibu Mkuu huyo alifafanua kuwa CCM miongoni mwa majukumu yake ni kuisimamia serikali itatue kero za wananchi hivyo haitokuwa tayari kuona vinafanyika vitendo vya kuharibu hali ya kisiasa na amani ya nchi  katika Mkoa huo.
“ Najua kuna watu wanafanya vitendo hivi kwa kuikomoa serikali na Chama ili wananchi wakose huduma za maji na kuilaumu serikali kuwa haitekelezi wajibu wake kwa jamii jambo ambalo sio sahihi.”, alisema Dk. Mabodi.
Alitoa wito kwa wananchi wa maeneo mbali mbali yenye miundombinu ya maji katika Mkoa huo kuhakikisha wanakuwa walinzi wa rasilimali hizo na kutoa taarifa sahihi kwa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) ili wawachukulie hatua za kisheria watu wanaijihusisha na hujuma hizo.
Naye Kaimu Afisa wa Maji wa Mkoa huo  wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Dude Juma Ame alishauri kuwekwa  walinzi katika maeneo mbali mbali yenye miundombinu ya maji katika Mkoa huo ili kudhibiti hujuma hizo.
Mapema akizungumza Naibu Katibu Mkuu huyo Dk. Mabodi  katika Kisima cha maji kilichopo maeneo ya Kitope Skuli ambacho hakitoi maji kutokana na  kuharibika kwa kifaa ndani ya Pampu ya kisima hicho aliwataka mafundi wa Mamlaka ya Maji  Zanzibar (ZAWA) kuharakisha matengenezo hayo ili wananchi wa maeneo hayo waendelee kupata huduma za maji.
Kutokana na mahitaji ya huduma ya maji safi na salama katika Hospitali ya Kitope,  Dk. Mabodi  alisema CCM Zanzibar  itachimba kisima cha maji safi na salama ndani ya hospitali hiyo ili wapate huduma hiyo kwa wakati mwafaka.
Akitoa ufafanuzi juu ya matengenezo ya Pambu ya Kisima hicho Afisa wa Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja, Amour Mohamed Silima alisema kuwa vifaa vinavyohitajika tayari vimeshapatikana hivyo kufikia kufikia mwezi  Novemba  4,  mwaka huu watakuwa wamekamilisha na wananchi wanapata  huduma ya maji.
Alifafanua kuwa changamoto inayowakabili katika miundombinu ya maji ndani ya Wilaya hiyo ni kuharibika kwa mashine za maji kutokana na athari za umeme zinazosababishwa na madhara ya Radi katika kipindi cha msimu wa Mvua za vuli zinazoendelea kunyesha nchini.
Ziara hiyo ya Dk.Mabodi ni ya kushutukiza baada ya kuwepo kwa malalamiko ya kukosa huduma ya maji kwa baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzbar akiwa katika ziara ya kukagua miundombinu ya Maji huko katika Kisima Cha Kitope Skuli Unguja akiwa ameongozana na viongozi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja  kushoto  Katibu wa CCM wa Mkoa wa Kaskazini Unguj, Mulla Othiman Zubeir na kulia ni Mwenyekiti wa CCM  Mkoa wa  Kaskazini Unguja Juma Haji.
chanzo:Zanzibar24

Comments