Wakili
Alex Balomi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mshtakiwa
Harbinder Sethi licha ya kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili na kuchukuliwa vipimo hadi sasa bado hajapa majibu wala
matibabu yoyote na afya yake inazidi kudhoofika.
Ameeleza
hayo leo Ijumaa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi mara baada ya
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kudai upelelezi wa
kesi hiyo bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine.
Kishenyi
baada ya kueleza hayo, Wakili Balomi alieleza kuwa kwa kiasi fulani
upande wa mashtaka umetekeleza amri ya Mahakama kwa kumpeleka Muhimbili
na kuchukuliwa vipimo lakini hajapewa majibu na wala hajatibiwa hadi
sasa.
Ameeleza
kuwa lile puto alilowekewa tumboni Sethi linatakiwa kubadilishwa
mwishoni kwa mwezi huu, lisipobadilishwa litageuka kuwa sumu na
kuhatarisha uhai wake.
Amesema daktari aliyechukua vipimo ampatie majibu ili aweze kujua hali ya afya yake ikoje.
Wakili
Kishenyi baada ya kutolewa kwa maelezo hayo amesema kuwa wao
wamekwishatekeleza amri ya mahakama, hawana cha kufanya zaidi kwa
sababu majibu ni siri ya magonjwa na daktari.
Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Takukuru, Leonard Swai yeye naye ameeleza kuwa suala la majibu ni suala la magonjwa na daktari.
Baada
ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Shaidi amesema amri ya Mahakama
imetekelezwa ambapo mshtakiwa alipelekwa Muhimbili na siyo jukumu la
Mahakama kuingilia kazi ya daktari hivyo alishauri mawakili wa upande wa
utetezi wafuate utaratibu.
Kesi imeahirishwa hadi Novemba 10, 2017 kwa ajili ya kutajwa na kuusisitiza upelelezi ukamilishwe.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments