Baadhi
ya wabunge wamehoji ni kwanini magari ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya
yanatangulia mbele huku ya kwao yakiwa ya mwisho katika msafara wa rais
pindi anapotembelea majimbo yao.
Hoja
hiyo imeibuliwa jana na Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilal (CCM),
wakati akichangia katika semina ya wabunge wa Kamati za Bunge kuhusiana
na masuala ya Kidiplomasia na Itifaki.
Naye
Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiku (Chadema), alihoji ni kwanini wao
huwa nyuma huku magari ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya yakipeperusha bendera
hoja iliyoungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso
(Chadema) huku Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah (CUF), akiomba apewe
ufafanuzi kuhusiana na mambo ya Itifaki.
“Katika
ziara hizo gari la Mkuu wa Mkoa huwa linaongoza mbele likiwa na bendera
na kufuatiwa na la Mkuu wa Wilaya kisha gari mbunge huwa la mwisho,
katika hili tunaomba ufafanuzi ni kwanini gari la Mbunge huwa ni la
mwisho katika ziara,” alihoji Hilal.
Mbunge
wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba (CCM), alipingana
na wabunge wenzake kwa kudai kuwa Mkuu wa Mkoa na Wilaya wana mamlaka ya
kupeperusha bendera kutokana na kuwa mteule wa Rais ambapo Rais
anachaguliwa na watu nchi nzima tofauti na mbunge ambaye anachaguliwa na
watu wa jimbo lake tu.
“Mkuu
wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya anamwakilisha Rais aliyechaguliwa nchi nzima
sisi ni vijimbo tu lakini pia wilaya yote ipo chini yake hata kama ni
majimbo matano lakini ndiyo viongozi pekee wenye kofia mbili ya kwanza
ukuu wa serikali wa eneo husika na pili ndiyo wenyeviti wa Kamati za
Ulinzi na Usalama katika maeneo yao,” alisema Mgumba.
Akitolea
ufafanuzi jambo hilo, Ofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Kitengo cha
Uhusiano wa Kimataifa, Ally Masabo alisema kiitifaki Mkuu wa Mkoa ndiye
anayetakiwa kuwa mbele kutokana na kuwa mteule wa Rais.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments