Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ameutembelea Mkoa wa Pwani kisha akatoa maagizo
mawili kwa uongozi na wananchi kuhusiana na mpango wa Serikali wa
kujenga Tanzania ya viwanda.
Katika
agizo la kwanza, Majaliwa amewataka viongozi kuboresha miundombinu ya
maeneo waliyoyatenga kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ili waweze kuwavutia
wawekezaji wa nje na ndani.
Alisema
kuwa ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa viwanda mkoani humo
na kuagiza wahakikishe maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji
yanakuwa na maji, umeme na barabara.
Kisha,
Waziri Mkuu aliwageukia wananchi waliopata ajira katika viwanda viwili
alivyovitembelea akiwataka wawe mabalozi wazuri wa Taifa kwa kufanya
kazi kwa uaminifu na uadilifu ili kuwathibitishia wawekezaji kwamba wana
uwezo mkubwa wa kazi na hakuna haja ya kutafuta wafanyakazi kutoka nje
ya nchi.
Majaliwa
alisema hayo jana alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na
wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza sabuni ya unga cha Keds kilichopo
Kibaha na kile cha vigae cha Twyford kilichopo Chalinze.
Alisema
mbali na viwanda hivyo kutoa ajira nyingi kwa Watanzania, pia
vitakapoanza uzalishaji vitawawezesha wananchi kupata bidhaa mbalimbali
kama vigae kwa bei nafuu kwa kuwa vitakuwa vinazalishwa nchini.
Awali,
Mkurugenzi Mtendaji wa viwanda hivyo, Jack Feng alisema ujenzi huo
umekamilika kwa asilimia 90 na sasa wako katika hatua za mwisho ikiwa ni
pamoja na ufungaji mitambo na vinatarajiwa kuanza uzalishaji Oktoba.
Mkuu
wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alimuomba waziri mkuu asaidie
upatikanaji wa nishati ya umeme ya kutosha kuweza kuendesha viwanda
katika mkoa huo.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments