Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuboresha
mikakati yake kwa ajili ya kudhibiti uchimbaji na biashara ya madini
nchini ili kuleta tija kwa maendeleo.
Majaliwa
aliyasema hayo jana wakati wa Mkutano wa 37 wa Mawaziri wa Nishati na
Madini wa nchi wananchama wa Kituo cha Madini cha African Minerals and
Geoscience Centre (AMGC), licha ya mambo mengine ulijadili mchango wa
sekta ya madini kwenye uchumi wa Afrika.
Waziri
mkuu alisema licha ya Tanzania kuwa na utajiri mkubwa wa madini, sekta
hiyo haina tija kwenye maendeleo ya uchumi kwa wananchi wake hasa
waishio karibu na migodi.
“Changamoto
kubwa ni namna tunaweza kuwa na sekta ya madini, inayoweza kutoa
mchango stahiki na kuwafanya wananchi wote kunufaika na kupata
maendeleo,” alisema Majaliwa.
Alisema hivi sasa hali hairidhishi kwa kuwa maeneo mengi ya machimbo yameharibiwa, huku wakazi wake wakiachwa maskini.
“Mfano,
Tanzania licha ya kuwa tajiri wa madini ya dhahabu, almasi, tanzanite,
shaba na chuma, mchango wa sekta hiyo ni asilimia 4.8 tu ya pato la
Taifa, hivyo kuna haja ya kuongeza usimamizi,” alisema.
Pia,
alihimiza kutumia kituo hicho kwa ajili ya kufanya utathmini na
uongezaji thamani wa madini nchini, badala ya kuyasafirisha yakiwa
ghafi.
“Kituo
hiki (AMGC) kinafanya utafiti, kinafundisha wataalamu na kina maabara
za kisasa kwa ajili ya uhakiki na uongezaji thamani madini,” alisema
Wakati
huohuo, Naibu Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema aliagiza
kampuni za madini na wachimbaji wadogo mwakani zitaanza kupeleka madini
kwa ajili ya kufanya tathmini ya viwango, badala ya kuyasafirisha nje ya
nchi.
“Nitoe
wito kwa kampuni zote za madini zianze kuleta madini yao katika kituo
hiki, ili yaanze kutathminiwa, badala ya kupeleka nje ya nchi,” alisema
Dk Kalemani.
Dk
Kalemani alisema, hatua hiyo ni utekelezaji wa msimamo wa Serikali wa
kudhibiti madini na kutaka yafanyiwe uchenjuaji na uongezaji thamani ili
kuongeza pato la nchi.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa AMGC, Ibrahim Shaddad alisema kituo hicho kinaundwa
na nchi nane wanachama na kwamba, wanatarajia kuzipokea nchi nyingi
zaidi kwa ajili ya kuimarisha utendaji.
Katika
Mkutano huo,Tanzania ilikuwa Mwenyekiti ambapo ulihudhuriwa na
Mawaziri,Makatibu Wakuu,Wakurugenzi kutoka Wizara ya madini pamoja na
Mashirika mbalimbali ya Kimataifa sanjari na kuadhimisha miaka 40 tangu
kuanzishwa kwa kituo hicho mwaka 1977.
chanzo:mpekuziblog.
Comments