
Watuhumiwa hao ni Ali Nyoro Tilima (32), Asha Mohamed Yussuf (30) wote wakaazi wa Wawi Chake Chake na Salum Said Kombo (23) mkaazi wa Konde Wilaya ya Miceweni Pemba.
Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Sheikhan Mohamed Sheikhan alisema kuwa, tukio hilo lilitokea jana saa 11:00 jioni katika maeneo ya Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) Chake Chake.
“Watuhumiwa hawa tuliwakamata maeneo ya PBZ Chake Chake ambapo ndipo kwenye makabidhiano yao, hivyo tuliangalia ndani ya DVD na tukagundua kete 969 za madawa ya kulevya”, alisema Kamanda huyo.
Kamanda Sheikhan alisema kuwa, wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na baada ya muda mfupi watapelekwa mahakamani.
“Tataendelea kumsaka mmoja mmoja ili kuhakikisha tunatokomeza janga hilo na tayari mtandao wote tunao na hata ule wa Unguja ambao unaleta madawa hayo tumeugundua na tayari tushakabidhi kwa muhusika wa madawa ya kulevya kitengo cha Makao Makuu”, alisema Sheikhan.
Kamanda huyo aliwataka wamiliki wa makampuni ya Meli kuwaonya mabaharia wao, kuacha tabia ya kusafirisha madawa ya kulevya, kwani wamekuwa ni msaada mkubwa wa kusafirisha madawa hayo.
“Tunayo orodha yote ya mabaharia wanaotoa msaada wa kusafirisha madawa ya kulevya na tukimbana hatua kali zitachukuliwa dhidi yake”, alieleza Kamanda.
Akizungumzia kukamatwa kwa wanawake wanojihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya, aliwataka waache biadhara hiyo kwani ina athari kubwa kwao na badala yake warudi katika nyuma katika mifumo ya kimaadili, ili kujipatia kipato halali cha kuendesha maisha yao.
Wanawake wawili wamekamatwa wakisafirisha madawa ya kulevya Mkoa wa Kusini Pemba ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, ingawa kisiwani Pemba ilikuwa ni jambo geni kukamatwa mwanamke na madawa ya kulevya.
chanzo:zanzibar24..
Comments