
Akizungumza katika Tamasha la kumi na moja la asasi za kiraia
Zanzibar Naibu katibu Mkuu Wizara ya katiba,Sheria,Utumishi wa Umma na
Utawala bora Mashaka Kubingwa Simba amesema uwepo wa asasi za kiraia
nchini unasaidia katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya
serikali hivyo ni vyema kuwa makini katika utekelezaji huo kwa
kufuata misingi ya utawala bora.
![]() |
Aidha amesema katika kutekeleza misingi ya utawala bora katika
jamii serikali imeweka mipango madhubuti katika kupambana na suala la
rushwa na uhujumu uchumi ili kuziba mianya ya upotevu wa mali za umma
kwa lengo la kudumisha misingi ya utawala bora.
Akizungumzia suala la ugatuzi amewataka wanaasasi hizo
kuwashajihisha wananchi masuala ya ugatuzi kwani serikali imo katika
mchakato wa kuyatekeleza kupitia baadhi ya sekta zake ikiwemo
elimu,afya na kilimo.
Nae Mwenyekiti wa Mwavuli wa asasi za kiraia Zanzibar Asha Aboud Mzee
amesema asasi zimeweza kupata mafanikio makubwa tangu kuazishwa kwa
matamasha yake ikiwemo ni pamoja na ushirikishwaji mkubwa katika
mipango ya uchambuzi wa sera na sheria katika baadhi ya sekta za
serikali.
Hata hivyo amesema kuwa ni vyema serikali kutoa nguvu zaidi kwa
asasi hizo ili kuweza kuleta mafanikio na maendeleo kwa wananchi
kama ilivyodhana ya utawala bora nchini.
Mwenyekiti huyo pia ametoa wito kwa watendaji wa asasi za kiraia
nchini kutovunjika moyo katika kupigania haki za wananchi katika
kuleta dhana ya utawala bora na watumie misingi ya usawa na haki
katika kufanikisha hilo.
Kwaupande wake Mkurugenzi wa mfuko wa kusaidia asasi za kiraia
kutoka Dar es salamu Profesa Honest Ngowi amesema katika kuhakikisha
asasi hizo zinapanda chati katika kuleta maendeleo wamekuwa
wakizipatia nguvu azaki zote ili ziweze kutoa misaada zaidi katika
jamii kwa kukuza maendeleo na uchumi wa nchi.
Mapema wakichangia mada ya utawala bora nchini baadhi ya wadau
walioshiriki katika tamasha hilo akiwemo Abdul-wahid Sariboko kutoka
Suza,Khadija Abdul-haji kutoka Zanzibar youth forum wamesema nivyema
asasi za kiraia kuwa mstari wa mbele katika kutoa ushauri juu ya
mipango mbalimbali ya serikali kwalengo la kuleta ufanisi wa utawala
bora.
Hata hivyo wamesema asasi zihakikishe zinashiriki katika upangazi
wa mipango ya utekelezaji na upimaji wa tathimini ya utekelezaji wa
mipango hiyo hasa katika mipango ya elimu,afya bora,
chakula,malazi,ajira,uhuru na kuzingatia haki na usawa katika utendaji
wao wa kila siku.
Aidha wamesema katika kutekeleza azma ya utawala bora lazima mambo
muhimu yafanyiwe kazi kama vile rushwa,udhalilishaji,migogoro ya
ardhi,mfuko wa haki jinai kuwa rafiki kwa jamii ya watu wenye ulemavu
pamoja na kutafutiwa ufumbuzi wa ucheleweshwaji wa kesi mahakamani.
Tamasha hilo la kumi na moja la asasi za kiraia litafanyika siku
mbili ambapo litajadili mambo mbalimbali ya utawala bora ambapo kauli
mbiu yake ni misingi ya utawala bora na ustawi wa asasi za kiraia
Zanzibar.

Comments