Utetezi wa Serikali Kuhusu kesi ya mamlaka ya wakuu wa mikoa na wilaya Kuwaweka Watu Mahabusu kwa saa 48.
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), amewasilisha utetezi dhidi ya kesi ya kupinga
mamlaka ya wakuu wa mikoa na wa wilaya kuamuru watu kuwekwa ndani kwa
saa 48, kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Pamoja
na maelezo ya utetezi, Serikali pia imewasilisha pingamizi la awali
dhidi ya kesi hiyo ikiiomba Mahakama iitupilie mbali hata kabla ya
kuisikiliza.
Kesi
hiyo ya Kikatiba namba 16 ya mwaka 2017 imefunguliwa na mwanasheria wa
kujitegemea, Jebra Kambole dhidi ya AG, akidai ni kutokana na kukithiri
kwa matukio ya wakuu wa mikoa na wilaya kuamuru watu kuwekwa mahabusu
kwa saa 48.
Mwanasheria
huyo anahoji uhalali wa vifungu vya 7 na 15 vya Sheria ya Tawala za
Mikoa Sura 97 ilivyorekebishwa mwaka 2002 vinavyowapa wakuu hao wa mikoa
na wa wilaya mamlaka hayo, akidai vinatumiwa vibaya bila kujali mipaka,
sababu, wala bila fursa ya kumsikiliza.
Kambole
ambaye anawakilishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na
Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), anaiomba Mahakama itamke kuwa
vifungu hivyo vinakiuka haki za binadamu zinazotolewa na Katiba ya nchi.
Amezitaja
haki zinazokiukwa kutokana na utekelezaji wa vifungu hivyo kuwa ni
uhuru wa kujieleza, usawa mbele ya sheria, utu na haki ya mtu kuwe huru
na kwenda mahali kokote atakako kinyume cha ibara za 12, 13(6)(a)(b)(e),
15 na 29 (1) za Katiba.
Hata
hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika majibu yake amesema vifungu
hivyo havikiuki haki hizo zinazotolewa na Katiba ya nchi bali vinaenda
sambamba na Katiba.
Pia, ameweka pingamizi la awali akiiomba mahakama iitupilie mbali kesi hiyo.
Katika
sababu zake za pingamizi la awali, anadai kesi hiyo haileweki na ni
batili kisheria kwa kuwa inakiuka kifungu cha 4 na cha 8 cha Sheria ya
Utekelezaji wa Wajibu na Haki za Msingi na kwamba haina maana na ni ya
kuudhi.
Pia,
anadai kiapo kinachounga mkono hati ya maombi ya faragha hakina mashiko
kwa sababu kinakiuka Amri XIX ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya
Madai.
Katika
maelezo yake ya utetezi, pamoja na mambo mengine anadai vifungu hivyo
vinatoa utaratibu mzuri kwa wakuu wa mikoa na wa wilaya wa kutekeleza
majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Anabainisha
kuwa, vifungu hivyo vinawapa wakuu wa mikoa na wa wilaya mamlaka kwa
mambo yanayohusu uvunjifu wa amani na utulivu kwa umma pale uvunjifu huo
unapokuwa hauwezi kuzuiliwa kwa njia nyinginezo zaidi ya kumweka
kizuizini mtu husika.
Anadai
makosa yote yanachunguzwa, yanashtakiwa na kushughulikia kwa mujibu wa
masharti ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, isipokuwa tu pale
ambapo sheria inaelekeza vinginevyo.
AG anadai masuala yanayohusu dhamana chini ya Sheria ya Tawala za Mikoa yanaongozwa na Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments