Wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanatarajia kunufaika na Mradi wa Ujenzi wa vyoo vinavyoendana na mahitaji yao mradi ambao unatekelezwa na Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto unicef, katika skuli za msingi hapa Zanzibar.
Akizungumza katika Uzinduzi wa Miongozo ya Maji ,Usafi wa Mwili na Mazingira Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Sefu Ali Iddi amesema Serikali kwa kushirikiana na shirika la Unicef watahakikisha mradi huo unawanufaisha wanafunzi kwa wakati.
Amesema kutokana na sekta ya elimu kukabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo uhaba wa vyoo katika skuli nyingi, hivyo uwepo wa mradi huo utasaidia kuondoa tatizo hilo kwa wanafunzi hususani wanafunzi wa kike na wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Aidha Balozi seif amesema Serikali itaendelea kuthamini na kutunza miradi ya maendeleo inayoanzishwa hapa Zanzibar ili iweze kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu katika kuwatatulia matatizo yanayowakabili.
Hata hivyo ametowa wito kwa taasisi za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Maji Zanzibar ZAWA kuimarisha ushirikiana katika utekelezaji wa Mradi huo ili maradi uweze kufikia malengo yaliokusudiwa ikiwemo kutatua matatizo ya ukosefu wa vyoo na maji safi katika skuli.
Akisoma hutuba ya Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto unicef kwa Niaba ya Mwakilishi wa UNICEF Tanzania, Rene Van Dongen amesema kutokana na Skuli za Zanzibar kuwa na Idadi kubwa ya wanafunzi na kusababisha uhaba wa miundominu shirika hilo litaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kusaidia sekta ya Elimu.
Hata hivyo amesema mradi huo pia utasaidia kuwanusuru wanafunzi kujikinga na maradhi ya mripuko yayoweza kujitokeza skulini mwao kutokana na vyoo viliopo skulini kutumiwa na idadi kubwa ya wanafunzi.
Amesema licha ya mradi huo kujenga vyoo 59 kwa skuli 27 za hapa Zanzibar ,mradi huo pia umelenga kuendelea kujenga vyoo katika skuli kumi katika mwaka wa Fedha 2017/18.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pembe Juma amewataka wadau wa maendele kuendelea kuisadia sekta ya elimu katika ujenzi wa Miundombinu ya kisasa ili wanafunzi waweze kupatiwa elimu inayoendana na mahitaji ya soko la Ajira.
chanzo:Zanzibar24.
Comments