Watu wamekuwa wakitupa takataka hovyo katika sehemu mbalimbali na kusababisha uchafuzi wa mazingira, bila ya kujua zinaweza kuwaingizia kipato kama wakizitunza vizuri.
Takataka zinazokusanywa sehemu mbalimbali huweza kuwa chanzo cha mapato kwa asilimia 100, kwa sababu ni kazi isiyohitaji mtaji wala kuwa na hasara.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kajenjere inayozoa taka jijini Dar es Salaam, Mathew Andrew alisema gari moja la taka hubeba kati ya tani 26 na 24, huku fedha inayopatikana kupitia taka hizo ni kuanzia Sh150,000 hadi Sh300,000 kwa kima cha chini. “Watu wasichokifahamu ni namna ya kuzihifadhi, unapozichanganya takataka zote katika sehemu moja unashusha tahamani yake, unatakiwa kuzitenga kila aina ya taka sehemu yake,” alisema Andrew.
Alisema katika utendaji wao wanapokusanya taka na kuzimwaga katika gari, baadhi ya vijana hufanya kazi ya kutenganisha ili kuchambuzi na kujua mahitaji ya soko ya kila aina.
Naye Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu alisema mpaka sasa katika halmashauri hiyo kuna kampuni saba zilizopewa zabuni ya kufanya usafi katikati ya mji, huku pembezoni wakitumia vikundi mbalimbali.
“Kampuni za sasa zina uwezo mkubwa na vifaa vya kisasa vya kufanyia usafi, hali ni tofauti na zamani hata ukiangalia katika soko la Kariakoo ni tofauti, kulikuwa na mlundikano wa taka kwa baadhi ya maeneo,” alisema.
Alisema usafi unaofanyika eneo la katikati ya jiji na hata mandhari ya bustani zinapendeza.
chanzo:Mwananchi.
Comments