CCM imeanza mchakato wa uchaguzi wa
viongozi wake kuanzia ngazi ya shina na sasa umefikia wilayani ambako
majina ya wagombea yanachujwa na vikao vya juu ambavyo vinafanyika
jijini Dar es Salaam kuanzia jana hadi mwishoni mwa wiki.
Baada
ya Kamati Kuu kumaliza vikao vyake vya siku mbili leo, CCM itakuwa na
kikao cha Halmashauri Kuu ambayo itabariki mapendekezo ya chombo hicho
cha utendaji cha chama hicho tawala.
Hakuna taarifa zilizotolewa jana kuhusu maazimio ya kikao hicho na juhudi za gazeti hili kupata wahusika ziligonga mwamba.
Matokeo
yake, usiri huo uliibua ubashiri ulioenezwa katika mitandao ya kijamii
kuwa wabunge wachache ambao wamekuwa wakionekana kuikosoa Serikali,
wamevuliwa uanachama.
Hata hivyo, gazeti hili halikuweza kuthibitisha habari hizo.
Picha
zilizotumwa na Ikulu jana zinaonyesha wajumbe wa kamati hiyo wakiwa
wamesimama kabla ya kuanza kikao, bila ya kuwapo katibu mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana.
Picha moja inamuonyesha Rais
Magufuli akiingia kikaoni, akiwa ameongozana na naibu katibu mkuu wa
CCM-Bara, Rodrick Mpogolo ambaye anaonekana kuwa ndiye aliyeshika nafasi
ya Kinana.
Mpogolo pia anaonekana pembeni ya Magufuli
ndani ya kikao kuthibitisha kuwa alishika nafasi ya Kinana sehemu fulani
ya kikao hicho.
Hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu kutokuwepo kwa mtendaji huyo mkuu wa CCM na kama aliingia kikaoni baadaye.
Picha nyingine inamuonyesha Waziri Mkuu wa zamani, Salim Ahmed Salim, ambaye huenda alikaribishwa kuhudhuria kikao hicho.
Salim
na marais wa awamu tatu zilizotangulia kabla ya Serikali ya Jakaya
Kikwete, ndiyo waliofanya kazi kubwa ya kutuliza wajumbe wa Halmashauri
Kuu mwaka 2015 wakati zogo lilipoibuka kutokana na jina la Edward
Lowassa kuenguliwa na Kamati Kuu kuwania kugombea urais kwa tiketi ya
CCM.
Habari ambazo Mwananchi ilizipata jana zinaeleza
kuwa Kamati Kuu ilianza kwa kupokea taarifa ya Kamati ya Maadili kuhusu
mwenendo wa wagombea wakati wa mchakato wa kuchukua fomu hadi sasa.
Taarifa
hiyo ndiyo inayotumiwa na Kamati Kuu kupitisha au kuondoa wagombea,
ambao hawakuruhusiwa kujitangaza, kujipitisha kwa wapigakura wala
kutumia mbinu nyingine yoyote kutafuta kura hadi watakapotambulishwa
mbele ya wapigakura.
Pia ripoti hiyo itawaweka bayana wanachama ambao wamesukumwa na watu wenye fedha ili wawatumie kwa malengo binafsi baadaye.
Pia,
taarifa zinasema mchujo huo utawagusa wale waliotahadharishwa kugombea
kutokana na vitendo vyao vya ukuikwaji wa maadili ndani ya chama.
Taarifa
zinaeleza kuwa licha ya kuweka miiko ya kugombea uongozi ndani ya
chama, kama kuwakataza watumishi wa Serikali kugombea nafasi ambazo
baadaye zitawalazimu kusimama kwenye majukwaa ya kisiasa kunadi sera za
chama, bado baadhi walijitokeza kugombea na kupitishwa na vikao vya
ngazi za chini.
Kikao hicho pia kinaangalia maadili ya
walioomba kugombea ili kuepuka kupitisha wagombea ambao ni watuhumiwa wa
ubadhirifu wa mali za chama, wasio wakazi wa maeneo husika na
waliopitishwa baada ya wengine kuonewa katika uteuzi na kuwapo mgombea
mmoja pekee aliyepitishwa badala kuwa na ushindani.
chanzoMwananchi.
chanzoMwananchi.
Comments