Kushuka au kupanda kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania hakutokani na kuruhusu bidhaa na huduma kutozwa kwa Dola, bali kunatokana na misingi ya shughuli za kiuchumi, Bunge limeelezwa.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashantu Kijaji ametoa kauli hiyo bungeni akijibu swali la mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga.
Mbunge huyo alitaka kujua hatua ambazo Serikali inatarajia kuchukua ili kuimarisha Shilingi ya Tanzania na kupiga marufuku matumizi ya fedha za kigeni nchini.
Naibu waziri alitaja sababu za kushuka kwa thamani ya Shilingi ni nakisi ya urari wa biashara ya nje ya nchi ambayo husababisha sarafu ya Tanzania kushuka thamani kama mauzo ya bidhaa ya nje.
“Hali hiyo hufanya thamani ya Shilingi kushuka kwa sababu ya mahitaji yetu ya fedha za kigeni ni makubwa kuliko mapato ya mauzo yetu nchi za nje, lakini pia mfumuko wa bei ambapo husababishwa na ujazo wa fedha kuliko uzalishaji,” amesema.
Dk Kijaji amesema sababu nyingine ni tofauti ya misimu ya upatikanaji wa fedha za kigeni kutokana na biashara za msimu kusababisha kuserereka kwa Shilingi.
Naibu waziri alitoa mfano wa Afrika Kusini akisema pamoja na sheria ya kutokutumia kabisa fedha za kigeni lakini sarafu ya nchi hiyo imepatwa na misukosuko mikubwa zaidi ya Shilingi ya Tanzania.
Dk Kijaji amesema mtikisiko upo hata kwa sarafu nyingine kubwa kama vile Yen ya Japan, Yuan ‘Renminbi’ ya China na Euro ambazo zimekuwa zikiyumba kwa kasi kuliko Shilingi ya Tanzania.
Comments