Wakati
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) akiendelea na
matibabu katika Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi, Kenya, Jeshi la
Polisi limemtaka dereva wake, Adam na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk
Vincent Mashinji kuripoti Polisi Dodoma au Makao Makuu ya Upelekezi Dar
es Salaam.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, SACP, Giless Muroto alisema jeshi hilo
linamtaka devera wa Lissu na Katibu Mkuu wa Chadema kuripoti polisi ili
kufanya mahojiano nao.
“Popote
alipo dereva wa Lissu, Adam ajitokeze na afike Polisi Dodoma na Makao
Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam ili kutoa maelezo kuhusiana na tukio
kwani ndiye alikuwa pamoja na majeruhi,” alisema.
Kamanda
alisema kitendo cha kutoweka kwa dereva huyo na kujificha ni kosa la
jinai na kama kuna mtu au watu wanaomficha, wanatenda kosa la jinai,
wamfikishe Polisi mara moja bila kukosa kwa kuwa ni shahidi muhimu
katika upelelezi.
Kuhusu
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Mashinji, naye anatakiwa kuripoti kituo cha
polisi kutokana na hotuba aliyotoa juzi, ambayo iliwahamasisha wanachama
wa chama hicho popote walipo, kuwa wanatakiwa kuchangia damu, kitendo
ambacho ni uchochezi, na kinaamsha mshituko katika jamii.
Akizungumzia
upepelezi kuhusu Lissu kushambuliwa na risasi kati ya 28 hadi 32 na
tano kumdhuru, Kamanda alitoa mwito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu
wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi.
Kamanda
Muroto alisema Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na timu
ya upelelezi kutoka Makao Makuu ya Upepelezi kutoka Dar es Salaam,
linaendelea kufanya upelelezi wa kina ili kuwabaini waliohusika na tukio
hilo.
“Pia
taarifa zimetolewa mapema katika wilaya na mikoa jirani ili kufanya
misako na ufuatiliaji kulingana na taarifa zilizopo ndani ya jeshi
hilo,” alisema.
Wakati
upelelezi ukiendelea, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na
jeshi hilo kwa kutoa taarifa sahihi ili kufanikisha kuwabaini watu
waliohusika na tukio hilo la kumshambulia Lissu na matukio mengine.
Kamanda
pia aliwaonya wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuandika habari
za upotoshaji, uchochezi dhidi ya taasisi za serikali na baadhi ya
viongozi wa dola kuhusu tukio hilo, kuacha mara moja.
Alitoa
angalizo kwamba wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii, wanatenda kosa
kisheria waanze kuchukua tahadhari wasije tumbukia mikononi mwa sheria.
Aliwataka
wale wote wenye taarifa sahihi kuhusu tukio hilo la kushambuliwa Lissu
wajitokeze na watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi au kwa viongozi wa
serikali walipo na taarifa hizo zitafanyiwa kazi ili kukomesha vitendo
hivyo.
Aidha
alisema jeshi hilo limeyakamata magari manane aina ya Nishani Patrol na
yanafanyiwa uchunguzi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na taasisi nyingine kuhusiana na kuhusishwa na tukio la kujeruhiwa
kwa risasi Mbunge Lissu.
Lissu
ambaye ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alishambuliwa kwa
risasi Septemba 7, mwaka huu saa 7.30 Area D katika maghorofa ya Wakala
wa Majengo Tanzania (TBA) katika Manispaa ya Dodoma.
Uchunguzi
wa awali kuhusu tukio hilo, ambalo watu walioshambulia hawajulikani,
Kamanda Muroto alisema unaonesha kuwa wahalifu walikuwa na silaha ya
SMG/SAR kutokana na maganda ya risasi yaliyokutwa eneo la tukio.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments