Kwa takriban wiki tatu, ambazo
gazeti la The Citizen limekuwa likifuatilia kwa karibu, maduka hayo
yamekuwa hayafanyi shughuli hizo za kubadilisha fedha na watu wa ndani
wamedokeza kuwa idadi inaweza kukua hadi kufikia maduka 100 kutokana na
kukaribia kwa tarehe ya mwisho kabla ya masharti hayo kuanza kutumika.
Kwa
mujibu wa The Citizen, maduka ambayo yamefungwa kwa takriban wiki tatu
ni pamoja na Ruby, Maddy, Europa, Money Link, Nana na Tungwe.
Hata
hivyo, haikuweza kuthibitisha mara moja kama kufungwa kwa maduka hayo
ni moja kwa moja au ni kwa muda na kama ni matokeo ya kuanzishwa kwa
masharti hayo mapya ya kupata leseni ya kuendeshea biashara hiyo au la.
Mkurugenzi
wa Benki Kuu Tanzania (BoT) anayehusika na usimamizi wa benki, Kennedy
Nyoni alisema juzi kuwa maduka yapatayo saba yameitaarifu taasisi hiyo
kuu ya kifedha nchini kuwa yanaachana na biashara hiyo ya ubadilishaji
fedha, lakini hakuwa tayari kuyataja.
Mmoja wa watu
wanaoendesha biashara hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliiambia
The Citizen kuwa masharti mapya ya utoaji leseni ni magumu kwa
wanaoendesha biashara ya ubadilishaji fedha na kukisia kuwa idadi ya
maduka yatakayofungwa inaweza kuongezeka hadi kufikia 100.
“Kusema
kweli, baadhi yetu tuko hapa kwa sababu tu bado tuna mikataba na
upangaji kwenye majengo tunayoendeshea biashara,” alisema mfanyabiashara
huyo.
“Mara tu mkataba utakapoisha, nasi pia tutafunga.”
Alisema
sharti kwamba anayetaka leseni ya biashara hiyo ni lazima aweke dhamana
ya Sh300 milioni halina uhalisia kwa sababu kipato anachoweza kupata
kirahisi ni Sh8 milioni tu katika kipindi cha miezi mitatu kwa kuwekeza
kiwango kama hicho cha fedha katika akaunti maalumu ya benki ya
biashara.
“Kwa nini mtu apitie mchakato mgumu wa
kutafuta Sh300 milioni na baadaye alipe kodi ya pango, na ajira katika
kipindi hiki ambacho biashara si nzuri?” alihoji.
“Kwa nini usiweke fedha hizo katika akaunti maalumu ya benki na kupata riba bila ya kutoka jasho?”
Lakini Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu aliiambia The Citizen kuwa masharti hayo hayatabadilishwa.
“Waendeshaji
wote wa maduka ya kubadilishia fedha wameshataarifiwa mabadiliko
yaliyofanywa katika kiwango cha mtaji kinachotakiwa na wanategemewa kuwa
wameyazingatia kabla ya tarehe ya mwisho kufika,” alisema Profesa
Ndulu.
BoT ilipitia upya kanuni zinazosimamia
uendeshaji wa maduka ya kubadilishia fedha nchini mwezi Juni, ikiwa ni
mpango wa kukabiliana na utakatishaji fedha.
Kumekuwa na tuhuma kuwa maduka hayo yamekuwa yakitumiwa na wafanyabiashara na viongozi wa Serikali kutakatisha fedha.
Kutokana
na kupitia upya kanuni hizo, BoT ilipandisha kiwango cha mtaji cha
uanzishaji maduka hayo, kuzuia utoaji wa leseni kwa maduka mapya na
kutaka wanaoendesha biashara hiyo kuomba upya leseni.
“Kiwango
kipya cha mtaji kimeongezwa kutoka Sh100 milioni hadi Sh300 milioni kwa
maduka ya daraja ‘A’ na kutoka Sh250 milioni hadi Sh1 bilioni kwa
maduka ya daraja ‘B’,” BoT ilisema katika mwongozo wake kwa maduka hayo
uliotolewa Juni 21.
Agosti 28, BoT iliongeza muda kwa waendeshaji maduka hayo kutekeleza maagizo hayo kuanzia Septemba hadi Desemba.
“Hii
ni kuwajulisha waendeshaji wote wa madula ya kubadilishia fedha kwamba
BoT imeongeza muda wa kuomba upya leseni hadi Desemba 31, 2017,” unasema
mwongozo huo wa benki hiyo.
Pia, ulitaka waendeshaji biashara hiyo kuhakikisha wanazingatia kiwango cha chini cha mshahara.
Kwa mujibu wa BoT, theluthi mbili ya mtaji huo inatakiwa iwe fedha taslimu.
chanzo:Mwananchi.
chanzo:Mwananchi.
Comments