Jaji
Mkuu Profesa Ibrahim Hamis Juma, ametoa angalizo kwa Majaji wafawidhi
kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii katika mahusiano pamoja
na kutoa michango kwenye mitandao hiyo juu ya jumbe zisizofaa.
Jaji Mkuu ametoa angalizo hilo wakati akifunga mkutano wa Majaji wafawidhi wa kanda nchini, uliofanyika Jijini Arusha
"Katika
suala la matumizi ya mitandao, kuweni makini. Msi- like picha ambazo
hazina maadili au kuchangia kwa kutoa maoni katika mitandao ya kijamii,"
alisema.
Aidha, amewataka kuwa makini na ndugu au jamaa wanaowatembelea, akisema baadhi yao wanatuhumiwa na makosa mbalimbali ya kijinai.
Aliwataka
majaji hao kujenga tabia ya kupenda kujisomea na kuelewa mabadiliko
yanayofanywa na Bunge kwa kurekebisha sheria ili kuweza kugundua makosa
mbalimbali yanayofanywa na Mahakama za chini na wafundishane namna ya
kuboresha hukumu zinazotolewa ili kupunguza mrundikano wa mashauri.
"Ni
vizuri kuelewa mabadiliko yanayofanywa na Bunge wakati wa kurekebisha
sheria, kazi na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa katika kufungua
mashauri," alisema.
Kuhusu
migongano kati yao na vyombo vingine vya serikali, aliwataka kutambua
mipaka ya vyombo hivyo na wao watambue mipaka yao huku akisisitiza
kwamba kila chombo kikitambua mipaka yake wataheshimiana na hakutakuwa
na mgongano katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mkutano
huo wa majaji wafawidhi ulikuwa mahususi kutathmini na kuweka mikakati
ya kumaliza mrundikano wa mashauri 2,198 yaliyopo Mahakama Kuu na
Mahakama ya Rufani, kati yao mengine yamekaa zaidi ya miaka 10.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments