Profesa Maghembe ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), kupitia hifadhi hiyo kuhakikisha hilo linatekelezwa.
"Ni
marufuku mtu yeyote kuonekana akilima katika eneo hili, wekeni askari
hapa, atakayeonekana piga pingu, hatuwezi kushuhudia watu wanalima ndani
ya hifadhi tukae kimya, ni lazima tuchukue hatua. Watangaziwe na wapewe
muda wa kuondoa mazao yao, ndani ya siku 30 au 40 wawe wameshaondoka,"
ameagiza waziri.
Agizo hilo amelitoa akiwa ziarani
katika hifadhi hiyo iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha kukagua
shughuli zinazofanywa na hifadhi, ikiwemo maeneo yenye mgogoro kwa ajili
ya kuyatafutia ufumbuzi.
Awali, akiwasilisha taarifa
kwa waziri, Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Steria Ndaga amesema eneo
hilo ambalo pia linajulikana kama shamba namba 40 na 41 limekuwa na
mgogoro tangu mwaka 1990 baada wananchi wa Kijiji cha Olkung'wado
kulivamia wakitoa hoja kadhaa, ikiwemo madai kuwa ni maeneo yao ya asili
waliyoyamiliki tangu zamani.
Amesema hoja nyingine
wanazozitoa wananchi ni kuwa, walipewa mashamba hayo na Serikali wakati
wa operesheni ya uanzishwaji wa vijiji mwaka 1975 na 1976.
Pia, wanadai hawakushirikishwa kwenye mchakato wakati wa ugawaji wa mashamba hayo na Tanapa haina hati miliki ya mashamba hayo.
Ngada
amesema hoja hizo zinakinzana na ukweli kuwa, shamba hilo
lilimilikishwa kwa Tanapa mwaka 1980 baada ya kutolewa tangazo kwa wadau
wanaoweza kuliendeleza kutokana na mwekezaji wa awali kushindwa
kuliendeleza, hivyo kufutiwa hati miliki na Rais mwaka 1979.
Amesema
wadau kadhaa waliomba umiliki wa shamba hilo ikiwemo Halmashauri ya
Kijiji cha Olkung'wado, lakini Kamati ya Ushauri ya Ardhi ya Mkoa wa
Arusha ikaishauri Serikali mashamba hayo yamilikiwe na Tanapa, hivyo
waliandikiwa barua ya kukubaliwa kupewa shamba na Idara ya Ardhi Mkoa.
Hata
hivyo, amesema katika kikao cha wadau wa uhifadhi kilichoitishwa na
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mei 11 iliazimiwa na kuridhiwa na Bodi ya
Wadhamini ya Tanapa kuwapa wananchi eka 366 ya shamba hilo na kubakiwa
na eka 600.
“Kikao pia kiliridhia Tanapa kuweka vigingi
vya mpaka katika shamba hilo, Mei 14 zoezi hilo lilianza na jumla ya
vigingi 26 viliwekwa,” amesema.
Hata hivyo, amesema
kumekuwepo taarifa kuwa baadhi ya wanakijiji wa Kitongoji cha Momella
walifungua kesi mahakamani wakidai Kijiji cha Olkung'wado
kimenyang'anywa ardhi na Tanapa.
Amesema Serikali ya kijiji imekana kwa maandishi kuhisika na ufunguzi wa kesi hiyo ikisema imefunguliwa na mtu binafsi.
Mkurugenzi
Mkuu wa Tanapa, Dk Allan Kijazi amesema maagizo yote aliyoyatoa waziri
ya kusitisha shughuli za kibinadamu ndani ya eneo hilo yatafanyiwa kazi
na atapewa mrejesho wa utekelezaji wake.
chanzo:Mwananchi.
chanzo:Mwananchi.
Comments