Lissu
ambaye ni mwanasheria wa Chadema ametimiza siku 13 tangu alazwe katika
Hospitali ya Nairobi (Nairobi Hospital) na hali yake inaendelea vizuri
baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7, nyumbani
kwake Area D mjini Dodoma.
Baada ya kumuona Lissu,
Zitto ambaye ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo alitumia mitandao ya kijamii
hasa ukurasa wa Facebook kuandika kwa kuanza na kichwa cha habari
‘Ujasiri’ kisha akaendelea kuandika, “Nimetumia wikiendi iliyopita
kumsabahi ndugu Lissu Nairobi. Nimerudi nikiwa mwenye unyenyekevu zaidi
kwa sababu ya nguvu na ujasiri ambao kaka yangu ameuonyesha licha ya
kuwa yupo kwenye maumivu makali.”
“Si mara nyingi hapa
nchini utasikia tukiongelea ujasiri. Lakini namfikiria Lissu na vile
nilivyojisikia nikiwa pamoja naye Nairobi. Najua hivyo ndivyo alivyo.
Waliomshambulia wamemuumiza.
Wamemuumiza kweli. Na bado wakati tuliokuwa naye amenionyesha shukrani, ari na ucheshi. Huo ni ujasiri.”
Wamemuumiza kweli. Na bado wakati tuliokuwa naye amenionyesha shukrani, ari na ucheshi. Huo ni ujasiri.”
Zitto
aliendelea kwa kuandika kuwa, “alichopitia na anachoendelea kupitia
Lissu siyo kitu rahisi kwa mtu yeyote, kutafakari na kufikiria hali ile
kungeniacha nimeumia moyo kama asingesema maneno haya kwangu:
‘Tumeshinda Tumeshashinda’.”
Mbunge huyo alimalizia kwa kuandika, “ujasiri ni Lissu.”
Wakati
Zitto akiandika hayo, juzi wabunge na meya wa Chadema walifanya ibada
ya kumuombea Lissu iliyofanyika jijini Nairobi katika Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri. Waliohudhuria ibada hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini,
Mchungaji Peter Msigwa, John Heche (Tarime Vijijini), Joshua Nassari
(Arumeru Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Meya wa Jiji la Dar
es Salaam, Isaya Mwita.
Baada ya kumalizika ibada
hiyo, Mchungaji Msigwa aliwashukuru wote walioonyesha mapenzi mema kwa
Lissu na kwa Chadema na kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kumuombea
mwanasiasa huyo na kutoa michango.
Wakati Mchungaji
Msigwa akieleza hayo, Lema alisema wakati huu umekuwa wa hofu, hivyo
aliwasihi watu wote wa Afrika Mashariki kumuomba Mungu aiondoe akigusia
pia uchaguzi Mkuu wa Kenya.
Kwa upande wake, Mwita
ambaye pia Diwani wa Vijibweni (Kigamboni), alisema wananchi wana kazi
ya kumuombea Lissu ili apone aweze kuendeleza mapambano ya kuwatetea.
Mbali
na viongozi hao wa Chadema na Zitto, wengine waliokwenda kumuona Lissu
ni Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman na Mbunge wa Singida
Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu.
Baada ya kumjulia hali, Nyalandu alisema Lissu alionyesha uso wa tabasamu, huku akimshukuru Mungu kwa kumruhusu kuwa hai.
Nyalandu
alieleza hayo kwa kutumia ukurasa wake wa Facebook kama ilivyo kwa
Zitto akiandika,“Muda mfupi uliopita nimeonana na Mh Lissu katika chumba
chake hospitali ya Nairobi na kuzungumza naye kuhusu hali yake na
anavyoendelea.”
“Ukweli ni kwamba ameumizwa vibaya.
Imeelezwa kwamba madaktari wanaendelea na hatua kadhaa za matibabu,
wakiwa wameanza kwa kumuimarisha (stabilization), ili kuufanya mwili
uweze kumudu hatua zaidi za utabibu anazopaswa kufanyiwa.”
Nyalandu
ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya
Awamu ya Nne alisema anaamini hatua zaidi na za haraka zitahitajika
kumsaidia ili apate huduma haraka za kitabibu katika ubora na ufanisi
uliopo kwa sasa duniani.
Wakati wabunge wa Chadema
wakipata fursa ya kumuombea Lissu jijini Nairobi, hapa nchini Baraza la
Vijana la Chadema (Bavicha) lilikwama kufanya maombi yaliyopangwa
kufanyika kwenye viwanja vya TP-Sinza baada ya polisi kufanikiwa kuzuia
mchakato huo.
Mbali na hilo, polisi iliwashikilia
vijana watano kwa mahojiano wakidaiwa kutaka kuandaa maombezi
yaliyopigwa marufuku kwenye uwanja huo.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Murilo Jumanne aliwaambia
wanahabari kwamba wenye nia ya dhati ya kufanya maombi au kuabudu wapo
katika makanisa na misikitini na siyo katika uwanja huo.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi alisema waliamua kufanya
maombi katika uwanja huo ili kuwapa fursa watu wa dini zote kujumuika.
“Hatukupanga
kumuombea Lissu peke yake, bali watu mbalimbali ikiwamo yule meja
jenerali mstaafu aliyeshambuliwa kwa risasi hivi karibuni. Pia kuliombea
Taifa kwa ujumla kutokana na vitendo vinayofanywa na watu
wasiojulikana,” alisema Katambi.
Mamilioni ya matibabu
Wakati hayo yakitokea watu mbalimbali wameendelea kuchanga fedha kusaidia matibabu ya Tundu Lissu.
Michango hiyo inatolewa baada ya Chadema kuomba msaada kwa yeyote anayeguswa ili kuhakikisha Lissu anapata matibabu bora.
Makamu
Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Profesa Abdallah Safari hivi
karibuni alieleza kuwa gharama za matibabu ya mbunge huyo ni Sh10
milioni kwa siku. Hadi jana jioni kwenye uchangishaji unaofanyika kwa
njia ya mtandao zilikuwa zimefikia takriban Dola18,000 za Marekani (sawa
na zaidi ya Sh39 milioni).
Mbali na hilo, taarifa
kutoka chanzo chetu kinachoaminika kilieleza kuwa Chadema wamepata
mchango wa Dola30,000 za Marekani kutoka nje ya nchi ambazo ni sawa na
Sh66 milioni.
Katika
mazishi ya Diwani wa Viti Maalumu Mbeya Mjini (Chadema), Ester
Mpwiniza, mbunge wa jimbo hilo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alimuomba
marehemu akamuombee kwa Mola mwanasheria mkuu wa chama hicho, Lissu ili
aweze kupona haraka.
Sugu alitoa maneno hayo jana jioni
wakati akielezea sifa na wasifu wa Mpwiniza ambaye aliwahi kuwa
mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha) Mbeya Mjini, alipokuwa akitoa
salamu zake kabla ya kufanyika kwa mazishi kwenye makaburi ya Sabasaba
jijini hapa.
Alisema anakipeleka kilio hicho kwa Mungu
kwa kuwa hali ya nchi ilipofikia sasa si salama akidai upinzani umekuwa
ukipata vikwazo vingi hata pale wanapofanya maombi ya pamoja, kujiombea
na kuiombea nchi amani wanazuiwa.
Pia, alisema licha ya
kuwa Mpwiniza alikuwa ngao kubwa katika ulingo wake wa kisiasa, pia
anaamini huko aendako atapokewa na malaika kutokana na kuyaishi maisha
ya upendo, ujasiri na kuwa mwanamke aliyethubutu kuwaunganisha wenzake.
“Nakuomba
dada yangu Ester naamini huko mbinguni umekwishapokelewa na malaika,
nakuomba dada nenda kwa Mungu muombe asimamie uhai wa Tundu Lissu,
amlinde na aponye haraka majeraha yake yaliyosababishwa na shambulio la
risasi. Mungu akuongoze kwenye sala,” alisema Sugu.
Mbali
na hilo, Sugu alitoa sifa kwa Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson
aliyehudhuria msiba huo bila kujali itikadi ya chama chake cha siasa na
kuonyesha dhahiri alivyo na mapenzi na ndugu zake wa Mkoa wa Mbeya.
Alisema
kuwa Dk Tulia alionyesha ukomavu wa kisiasa na kwamba, hizo ni salamu
tosha za kupeleka kwenye mamlaka nyingine ambazo badala ya kuwaunganisha
wananchi katika misiba, zinasababisha watu wengine waogope kuzikana
wakati kifo hakina itikadi.
chanzo:Mwananchi.
Comments