
Alhaj Dk. Shein alisema kuwa misikiti hiyo ya kisasa iliyojegwa kwa
gharama kubwa imekuwa ikipoteza haiba na kukumbwa na chamgamoto ya
uchakavu wa miundombinu muhimu baada ya kipindi kifupi tangu
inapokabidhiwa kwa Kamati za Misikiti au wananchi wa maeneo
yanayohusika.
Hayo ameyasema leo katika ufunguzi wa msikiti wa Jaamiu Zinjibar
ambapo katika hotuba yake ya ufunguzi wa msikiti huo , Alhaj Dk. Shein
alisisitiza kuwa kila inapowezekana ni vyema Ofisi ya Mufti ikawa na
ufuatiliaji wa misikiti hiyo inayojengwa kwa gharama kubwa ili kuangalia
utunzaji na maendeleo yake.
Aliongeza kuwa miradi ya ujenzi wa misikiti inayojengwa na ikatunzwa
vizuri na kwa uadilifu, huwa wanatiwa moyo wale wenye nia na ari ya
kusaidia na kuzidi kufungua milango ya kheri, neema na riziki kwa
Waislamu wa maeneo mengine ambao bado hawajafaidika na neema kama hiyo.
Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani za dhati kwa
Serikali ya Oman kwa kukubali kujenga msikiti huo mkubwa, mzuri na wa
kisasa hapa Zanzibar na kutoa shukurani kwa wananchi wa Oman chini ya
uongozi imara wa Sultan Qaboos Bin Said Bin Al Said.
Pia, Dk. Shein alimpongeza Balozi Mdogo wa Oman aliyopo Zanzibar Dk.
Ahmed Hamoud Al Habsi na wasaidizi wake kwa juhudi walizochukua hadi
mradi huo ukakamilika kwa ufanisi mkubwa kwa kushirikiana na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alisisitiza haja ya kuitumia misikiti ipasavyo
na kujiepusha kufanya mambo yanayoweza yakawa shirki sambamba na
kujiepusha na mizozo pamoja na mifarakano ambayo haina tija kwa
Waislamu.
Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa kwa bahati mbaya katika miaka ya hivi
karibuni, kuna baadhi ya Waislamu katika baadhi ya misikiti walianza
kugombania uongozi wa misikiti, walikuwepo waliotishia kuiteka misikiti
kwa kuwa katika himaya yao na baadhi yao walifanya uharibifu wa vifaa na
nyenzo.
Aliongeza kuwa wapo waliodiriki kuwafukuza waumini wenzao na kugawana
makundi ya waliokuwa na haki na wasiokuwa na haki ya kuongoza na
wengine walipoanzisha mizozo yao walidiriki hadi kupigana na kuumizana
kwani walighafilika juu ya umuhimu wa msikiti na mwenye msikiti.
Alieleza imani yake ni kwamba msikiti huo wa Jaamiu Zinjibar utakuwa
ni miongoni mwa kiungo muhimu cha kuwaunganisha Waislamu wa Zanzibar
kutokana na jina uliopewa na kuwa kitovu muhimu katika kutekeleza ibada
ya funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kukumbushana umuhimu
wakutekeleza Hijja.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwahimiza wananchi na waumini
wanapopata bahati ya kuwaleta wadhamini na wafadhili wa ujenzi wa
misikiti na madrasa na uchimbaji wa visima, wawafikishe wafadhili hao
katika sehemu za vijijini, Unguja na Pemba ili nao wazidi kupata neema
hiyo kwani misikiti na madrasa nyingi za kisasa bado zinajengwa katika
maeneo ya mjini ikilinganishwa na vijijini.
Pia, Alhaj Dk. Shein alitoa wito kwa Waislamu wote washirikiane
katika kujenga madrasa wao wenyewe badala ya kukaa na kusubiri wafadhili
katika kutekeleza ibada hiyo muhimu huku akiwataka wazazi kuwa na moyo
wa kushirikiana na walimu wa madrasa katika kusomesha na kuwalea watoto.
Nae Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mmanga Mjengo
Mjawiri alitoa pongezi kwa Serikali ya Falme ya Oman na hasa Sultan
Qaboos kwa msaada wa TZS Bilioni 17.9 ambapo Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imechangia eneo la ujenzi, msamaha wa kodi wa vifaa vyote vya
ujenzi vilivyotoka nje ya nchi na msamaha wa malipo ya mkandarasi sawa
na TZS Bilioni 3.1.
Mkataba wa ujenzi wa Msikiti huo ulitiwa saini tarehe 6 Januari mwaka
2014 baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyowakilishwa na
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Serikali ya Falme ya Oman
iliyowakilishwa na Ofisi ya Diwan of Royal Cort ambapo ujenzi umefanywa
na Kampuni ya Esteem Construction ya Dar-es-Salaam na kusimamiwa na
Wahandisi wa Ofisi ya Diwan of Royal Cort ya Oman.
Msikiti huo mkubwa una nafasi ya kusaliwa na Waislamu zaidi ya 4,000
na una sehemu ya kusali wanaume na wanawake, vyumba sita vya madarasa,
maktaba, maabara ya lugha na kompyuta, ukumbi wa mihadhara ya shughuli
za kidini pamoja na maegesho ya gari.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo msikiti huo wa kisasa ambao
unatarajiwa kuendesha ibada na pia kutoa mafunzo mbali mbali ya Dini ya
Kiislamu na lugha mbali mbali ikiwemo lugha ya kiarabu.
Mapema Mwakilishi wa Serikali ya Oman na Katibu Mkuu wa Kituo Kikuu
cha Sayansi na Utamaduni cha Sultan Qaboos, Habib bin Mohammed Al Riyami
alisema kuwa ujenzi wa msikiti huo ni njia moya wapo ya kujenga
uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Zanzibar na Oman na
kuahidi kuwa Oman chini ya uongozi wa Mfalme Qaboos itaendelea kuiunga
mkono Zanzibar katika kuendeleza sekta za maendeleo ikiwemo elimu pamoja
na kuiimarisha dini ya Kiislamu.
Mufti Mkuu wa Zanzibar Saleh Omar Kabi alieleza fadhila za kujenga
msikiti pamoja na kuendeleza elimu ya dini ya Kiislamu na kusisitiza
kuwa wananchi wa Oman wakiongozwa na Sultan Qaboos wameendelea kuonesha
udugu wa damu kati yao na wananchi wa Zanzibar kama ilivyokuwa kwa Aus
na Hazraj wakati wa Mtume Mohammad (SAW).
Viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali
ya Oman, Masheikh pamoja na wananchi walihudhuria katika ufunguzi wa
msikiti huo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Idd, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Balozi Mdogo wa Oman Dk.
Ahmed Hamoud Al Habsi na viongozi wengineo.
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk.
chanzo: zanzibar24.
Comments