Watanzania
watatu akiwamo dereva wa kampuni ya saruji ya Dangote, Khalid Abdallah
na wahamiaji wanane raia wa Ethiopia wamefikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano.
Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili ni kusafirisha kwa magendo binadamu na kuingia nchini kinyume cha sheria.
Mwendesha
Mashtaka wa Uhamiaji, Novatus Mlay amewasomea mashtaka hayo leo
Jumatano mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.
Baada ya kusomewa mashtaka, raia hao wa kigeni wamekubali makosa yote yanayowakabili, huku Watanzania wakikana.
Raia
hao wa Ethiopia, Solomon Ertiso, Gazahegn Tiroro , Haire Latso,
Thadius Lilanso, Dawit Habtam, Deznet Godebo, Feraru Gurana na Elioj
Akola wanadaiwa Septemba 20 katika eneo la Kongowe wilayani Temeke
walikamatwa wakiingia nchini bila ya kuwa na kibali.
Kwa
upande wao, Khalid Abdallah ambaye ni dereva wa kampuni ya Dangote;
Hussein Hamad Hassan na Jumanne Mtambo wanadaiwa Septemba 20 eneo la
Kongowe wakiwa raia wa Tanzania walikutwa wakiwasafirisha wahamiaji hao
haramu kimagendo.
Wanadaiwa
waliwasafirisha wahamiaji hao kwa kutumia gari mali ya kampuni ya
Dangote kwa kuwatoa Tanzania kwenda nchini Afrika Kusini.
Pia, wanadaiwa kuwaingiza ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania raia hao wa Ethiopia. Washtakiwa wamekana mashtaka.
Hakimu
amewataka kuwa na wadhamini wawili kila mmoja ambao watasaini bondi ya
Sh50 milioni kila mmoja. Kesi itatajwa Oktoba 10 na upelelezi imeelezwa
haujakamilika. Walishindwa kutimiza masharti hayo hivyo wamepelekwa
rumande.
Kwa upande wa raia wa Ethiopia, Mahakama imesema watasomewa maelezo ya awali Oktoba 10.
Wakati
huohuo, raia 31 wa Ethiopia na wawili wa Tanzania wamepandishwa
kizimbani mahakamani hapo wakikabiliwa na mashtaka matano ya kuingia
nchini kinyume cha sheria.
Raia hao wa kigeni walikubali mashtaka na watasomewa maelezo ya awali Oktoba 11.
Watanzania
Ibrahim Abdallah ambaye ni dereva wa gari aina ya Nissan Civilian na
kondakta Christopher Steven wanadaiwa Septemba 25 eneo la Toangoma
wilayani Temeke walikutwa wakiwasafirisha raia hao wa Ethiopia
kimagendo kutoka Tanzania kwenda Afrika Kusini.
Washtakiwa
walikana shtaka na upande wa mashtaka ulidai upelelezi haujakamilika.
Kesi itatajwa Oktoba 11. Washtakiwa wamepelekwa rumande kwa kushindwa
kutimiza masharti ya dhamana.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments