Alisema kuwa
familia ndiyo ilikuwa inakaa kikao cha kujadili taratibu za kusafirisha
miili na mazishi na kwamba taarifa kamili itatolewa leo.
Familia
ya Teu, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko
imepata msiba mzito kwa kuondokewa na baadhi ya wanafamilia katika ajali
iliyoua watu 13 iliyotokea nchini Uganda.
Familia hiyo
ilikwenda Uganda kwenye sherehe ya harusi ya ndugu yao na usiku wa
Septemba 17, 2017 wakati wakirejea Tanzania, basi lao liligongana na
lori katika barabara ya Mataka na kuwaacha watu wanane wakijeruhiwa
vibaya.
Kwa mujibu ya taarifa iliyotolewa na kusainiwa
na mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Gerson
Msigwa, Rais John Magufuli ametoa salamu za rambirambi kwa familia hiyo
kwa kupoteza wapendwa wao.
“Nimepokea taarifa ya vifo
hivi kwa mshtuko mkubwa, nimehuzunishwa na kuondokewa na idadi hii kubwa
ya watu, nampa pole Gregory Teu kwa kufikwa na msiba huu mkubwa, nawapa
pole wanafamilia, ndugu na jamaa wote walioguswa na vifo hivi.”
“Nawaombea
marehemu wote wapumzishwe mahali pema na pia nawaombea majeruhi wote
wanaopata matibabu huko nchini Uganda wapone haraka na kurejea
nyumbani,” amenukuliwa Rais Magufuli kwenye taarifa hiyo.
Rais
Magufuli amewataka wanafamilia wote kuwa na moyo wa subira, uvumilivu
na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa
wao na watu muhimu waliowategemea.
Awali, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema wanafamilia hao walipata
ajali wakiwa kwenye basi aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili
za Tanzania ambalo lilikuwa limetokea Uganda kuja nchini. “Ni kweli
tumefuatilia basi hilo na kubaini kwamba liliondoka hapa nchini Septemba
15 kwenda Uganda kwenye shughuli ya harusi. Mengine siwezi kusema zaidi
mpaka tutakapofanya mawasiliano na mamlaka za Uganda,” alisema Kamanda
Ollomi.
Gazeti la Uganda la Daily Monitor limeripoti
kwenye tovuti yake kwamba Watanzania hao walikwenda Uganda kwenye harusi
ya binti yao, Dk Annette Ibingira ambaye amefunga ndoa na raia wa
Uganda, Dk Treasurer Ibingira.
Majeruhi walipelekwa
hospitali ya Nkozi kwa ajili ya matibabu lakini baadaye walipewa rufaa
na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mulago. Maiti zote zilipelekwa
hospitali ya Gombe kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
chanzo:Mwananchi.
chanzo:Mwananchi.
Comments