Homa ya wamiliki wa nyumba zilizowekwa alama ya X
jijini Tanga imeanza kupoa baada ya maofisa wa Kampuni Hodhi ya
Rasilimali za Reli (Rahco), kupita mara ya pili na kuandika maneno imefutwa.
Ofisa
Habari wa Rahco, Catherine Moshi amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya
uongozi wa kampuni hiyo na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella
kufikia uamuzi kwamba busara itumike ili Jiji la Tanga lisitoweke.
“Maofisa
wetu wapo jijini Tanga wanapita kufuta alama ya X kwenye nyumba zilizo
kwenye mapishano ya reli ziliwekwa kwa umbali wa mita 100 na sasa
itapungua hadi mita 30,”amesema Moshi.
Moshi amesema
katika kikao na Shigella ilibainika isipotumika busara na sheria ya
kubomoa nyumba zote zilizo umbali wa mita 100 ikifuatwa kwenye makutano
ya reli, basi mji wa Tanga utatoweka na kubakiwa na nyumba chache.
Amesema kutokana
na hilo, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) italazimika kuweka taa kubwa na
vibao vyenye alama kuonyesha kuwa ni makutano ya reli.
Ofisa
huyo amesema sehemu nyingine yatajengwa mageti na watakuwepo watumishi
wenye bendera kuonyesha ishara wakati treni itakapokuwa ikipita.
Mwananchi
Digital imeshuhudia baadhi ya nyumba katika mitaa ya Chuda na Central
jijini Tanga ambazo zilikuwa zimewekwa alama ya X zikiwa na maandishi
ya njano yanayosomeka imefutwa.
Mkazi wa Chuda, Omari Jumaa amesema busara imewaokoa baadhi ya wenye nyumba, lakini bado kuna hofu kwa wengine.
chanzo:Mwananchi.
chanzo:Mwananchi.
Comments