
Akizungumza na Nipashe katika Hospitali ya Rufani ya Bugando jana,
Editha Malima (Esther Ntobi), alisema kabla hajapigwa risasi, yeye na
familia yake walikuwa wakila chakula cha usiku huku wakiangalia taarifa
ya habari kwenye televisheni lakini ghafla walisikia kishindo nje ya
nyumba na baada ya kutoka walikuta gari aina ya Toyota Hiace likiwa
limegonga nyumba yao.
“Baada ya kuona nyumba yetu imegongwa, mume wangu alipiga simu Polisi na muda si mrefu askari walifika,” alisema Editha.
“Mimi niliingia ndani, lakini muda kidogo nilisikia mume wangu akilia ‘mnaniua jamani, nisaidieni’.”
“Nilitoka nje nikaona askari saba wanampiga… nilienda
kuwaomba msamaha, lakini na mimi walinipiga hadi wakanivua nguo nikabaki
uchi wa mnyama.
“Nilifanikiwa kukimbia ndani na mume wangu, lakini walitufuata wakaanza kuwapiga na watoto.
“Niliwaomba wasiwapige watoto, lakini askari mmoja
alimwambia mwenzie mpige risasi, nililia nikiomba msamaha ndipo huyu
mwingine alinipiga risasi ya mguu na mwingine akanipiga na kitako cha
bunduki kidevuni.”
Editha alisema askari hao walipompakia kwenye gari la polisi
waliendelea kumpiga na kumfikisha kituoni huku damu zikiendelea kuvuja.
Alisema walipofika kituoni walimkalisha chini kwa vipigo ndipo Mkuu wa Kituo (OCS) cha Mabatini aliwakataza.
“Aliwaambia ‘msimpige huyu mama, hana kosa lolote’,” alisema.
“Niliandikiwa RB na kwenda hospitali (ya mkoa) ya Sekou
Toure, lakini ilishindikana, nilihamishiwa Hospitali (ya Rufani) ya
Bugando ambayo mpaka sasa naendelea na matibabu.”
Daktari bingwa wa mifupa katika Hospitali ya Rufani ya Bugando,
Izidoriy Ngaiyomela amethibitisha Editha kupokelewa hospitalini hapo
Agosti 9 majira ya saa 10:30 jioni akiwa na jeraha la risasi katika mguu
wake wa kulia.
Aidha, muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo, Leokadia Ngovongo alisema majeruhi huyo anaendelea vizuri na matibabu yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna Ahmad Msangi
aliwaambia waandishi wa habari juzi, kuwa amewasimamisha kazi askari
wanne wa Kituo Kikuu cha Nyamagana kwa tuhuma za kufyatua risasi ovyo na
kumjeruhi mke wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Majengo, eneo la
Mabatini.
Kamanda Msangi alisema askari hao ambao hakutaja majina yao, hawakutumwa na jeshi lake kufanya tukio hilo.
Alisema endapo itathibitika kuwa walifyatua risasi hizo kwa makusudi au uzembe, hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.
chanzo: zanzibar24.
Comments