
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Baroness Scotland
aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein Ikulu mjini
Zanzibar.
Katika maelezo yake Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa Jumuiya ya Madola
inaendelea kutekeleza mipango na mikakati kabambe ambayo imeiweka kwa
wanancha wake ikiwemo Tanzania ambapo Zanzibar pia, ni miongoni mwao.
Bi Scotland alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa
juhudi kubwa anazozichukua katika kuhakikisha Zanzibar inakuza uchumi na
kuimarisha amani na utulivu na kusisitiza kuwa Jumuiya anayoiongoza
haitokuwa nyuma kumuunga mkono.
Aidha, Bi Scotland alimueleza Dk. Shein miongoni mwa mipango ya
Jumuiya hiyo kwa nchi wanachama wake wote 52 ikiwa ni pamoja na kuongeza
fursa katika sekta ya biashara nan uchumi, kuwasaidia wanawake, vijana,
upatikanaji ajira kwa vijana, elimu, kutunza mazingira, uwezeshaji na
mengineyo.
Aliongeza kuwa uchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo umekuwa
ukiimarika kwa kiasi kikubwa kwa zile nchi za Bara la Afrika na hata
nchi za Bara la Asia uchumi wake umeimarika kwa asilimia 5 hadi asilimia
8.
Katika mazungumzo hayo, Bi Scotland alimueleza Dk. Shein kuwa
miongoni mwa maeneo yaliopewa kipaumbele na Jumuiya hiyo ni katika
kuhakikisha nchi zake wanachama zinaimarika kiuchumi ni pamoja na
miundombinu na nishati.
Akieleza juu ya Jumuiya hiyo ilivyoweka mikakati katika kusaidia
katika kupambana na changamoto ya hali ya mabadiliko ya tabia nchi hasa
kwa nchi za Visiwa, Bi Scotland alitoa mfano wa nchi yake ya kisiwa cha
Jamhuri ya Dominica jinsi ilivyopata athari zilizotokana na hali hiyo.
Nae Rais Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa kiongozi huyo
kwa ujio wake hapa Zanzibar sambamba na juhudi kubwa zinazochukuliwa na
Jumuiya hiyo katika kuendelea kuiounga mkono Zanzibar.
Dk. Shein kwa upande wake alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar iko
salama na usalama wake unatokana na kuwepo kwa amani na utulivu mkubwa
hatua ambayo inapelekea hata uchumi wake kuzidi kuimarika siku hadi
siku.
Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kupata
mafanikio makubwa katika kuimarisha uchumi wake kutokana na sekta ya
utalii, sekta ambayo bila ya kuwepo kwa amani na utulivu ni vigumu
kuimarika.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar jinsi inavyochukua hatua katika kuimarisha sekta za
maendeleo na kueleza azma ya ujenzi wa bandari mpya ya Mpiga Duri pamoja
na kuuimarisha uwanja wake wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume
kwa kujenga jengo jipya la abiria.
Aidha, Dk. Shein alieleza mafaniki yaliopatikana katika kuimarisha
demokrasia na utawala bora hapa nchini huku akimueleza juhudi
zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutunga
sheria ya maadili kwta viongozi wa umma.
Dk. Shein, pia, alitumia fursa hiyo kumueleza Katibu Mkuu huyo hatua
zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kupambana na vitendo vya
udhalilishaji wa akina mama na watoto sambamba na juhudi za Serikali za
kuanzisha Pencheni Jamii kwa wazee kuanzia miaka 70, jambo ambalo Bi
Scotland alilipongeza.
Pia, alimueleza hali ya mabadiliko ya tabia nchi jinsi inavyoathiri
mazingira ya Zanzibar hasa katika kasiwa cha Pemba na sehemu nyenginezo
na kueleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali pamoja na Jumuiya
za Kimataifa katika kupambana na hali hiyo huku akitolea mfano mkutano
wa nchi zinazoendelea za visiwa (SIDS) uliofanyika mwaka 2014 huko Samoa
na maazimio yake juu ya hali hiyo.
Akijibu masuali ya waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo, Bi
Scotland aliwataka wapinzani kushirikiana na Serikali anayoiongoza Dk.
Shein kwa lengo la kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wa Zanzibar na
kusisitiza kuwa Zanzibar inafaidika na misaada ya Jumuiya hiyo kupitia
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jumuiya ya Madola ilianzishwa karne ya 20 kwa lengo la kuikutanisha
Uingereza na yaliyokuwa makoloni yake duniani kwa jukumu la kuhakikisha
wanachama wake wanajikwamua katika Nyanja mbali mbali za kimaendeleo
ikiwemo kisiasa, kiuchumi, kijamii, michezo na burudani huku Malkia wa
Uingereza akiwa ndiye Kiongozi Mkuu wa Jumuiya hiyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
chanzo: zanzibar24.
Comments