DPP aachana na kesi ya ugaidi kwa mbunge wa CHADEMA Wilfred Lwakatare.

Mkurugenzi wa Mashtaka DPP ameondoa maombi yake juu ya Mbunge wa Bukoba Mjini wa Chadema, Wilfred Lwakatare kuhusiana na shtaka la ugaidi dhidi yake.
 
DPP alikuwa amefungua maombi Mahakama ya Rufani akiomba kibali cha kufungua maombi ya mapitio kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu kumfutia Lwakatare mashtaka ya ugaidi.
 
Maombi  ya DPP yalitarajiwa kusikilizwa leo Ijumaa, Agosti 11 na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mussa Kipenka, lakini wakili wa serikali Mkuu, Tumaini Kweka ameiambia mahakama kuwa DPP hana nia ya kuendelea na maombi hayo kutokana na uamuzi wake wa kuyaondoa maombi hayo kabla ya usikilizwaji.
 
Kutokana na hatua hiyo wakili wa mjibu maombi, Richard Rweyongeza amesema hana pingamizi dhidi ya maamuzi hayo ya DPP pia na Jaji Kipenka akatoa amri ya kuyaondoa mahakamani maombi hayo.
 
Hivyo kwa sasa Lwakatare anabaki na shtaka la kula njama ili kutenda kosa, katika kesi ya msingi inayosikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
 
Lwakatare na mwenzake Ludovick Rwezaura walikuwa wanakabiliwa na jumla ya mashtaka manne yakiwemo ya kufanya ugaidi na kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi kwa lengo la kumdhuru kwa sumu aliyekuwa Mhariri wa gazeti la Mwananchi, Denis Msacky.
chanzo: zanzibar24.

Comments