Ajali ya ndege yaua mkoani Arusha.

Mwanaume mmoja mkaazi wa Dar es salaam David Mbale mwenye miaka 25, amefariki dunia baada ya ndege aliyokuwa akiendesha kuanguka kwenye vilima vya Monduli mkoani Arusha.
 
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema tukio hilo lilitokea juzi katika Kijiji cha Engalaoni kilichopo mpakani mwa wilaya za Monduli na Arumeru.
 
Kamanda Mkumbo amesema Rubani huyo, alikuwa akiendesha ndege ndogo yenye namba za usajili 5HSAL 206 inayomilikiwa na Kampuni ya Safari Air Link.
 
“Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria watano, iliondoka katika uwanja mdogo wa ndege wa Arusha, majira ya saa 1:30 asubuhi siku hiyo ya tukio ikielekea katika eneo la Kogatende, Serengeti kuwachukua watalii.
 
“Kwenye ndege hiyo, alikuwamo rubani peke yake na alikuwa anasubiriwa na watalii huko Serengeti.
 
“Taarifa za kuanguka kwa ndege hiyo zilianza kuenea juzi saa nne asubuhi, zikisema kuna ndege imeanguka katika vilima vya Monduli ambavyo ni maarufu kama Monduli Hills.
 
“Baada ya taarifa hizo kutolewa saa 6:30, tuliwajulisha kikosi cha zimamoto na wenzetu wa uwanja wa ndege wa Arusha na walipofika kwenye kilima hicho, walikuta rubani ameshafariki dunia na mwili wake ulichukuliwa kwa uchunguzi zaidi,” alisema Kamanda Mkumbo.
 
Hivyo Kamanda Mkumbo amesema uchunguzi wa tukio hilo umeanza na watashirikisha na wataalamu waliobobea katika masuala ya ndege ili uchunguzi huo uende kiufasaha zaidi.
Chanzo: zanzibar24.

Comments