Wawili wafariki na 6 kulazwa baada kula ugali wa Muhogo Mkoani Rukwa.

Ugali wa Muhogo wawaua watu wawili wa familia moja katika kijiji na kata ya Kisumba tarafa ya Kasanga wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa na wengine 6 kulazwa katika zahanati ya kijiji hicho baada ya kula ugali wa muhogo.
 
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Diwani wa kata hiyo Innocent Kukongwa alisema watu hao walikula ugali wa muhogo ambao ulikuwa umeandaliwa kama chakula cha usiku ,ambapo baada ya kulawalianzakuharisha na kusababisha watoto wawili kufariki dunia na wengine sita kukimbizwa zahanati kwa matibabu zaidi.
 
Amefahamisha kuwa  baada ya kutumia chakula hicho waliamua kutumia dawa ya kienyeji badala ya kwenda hospitali na kusababisha kifo kwa watoto hao.”Inasikitisha kwani baada ya kula chakula hicho hawakutaka kwenda zahanati na badala yake waliendelea kujitibu kwa kutumia miti shamba na kushtuka baada ya kuona hali bado ilikuwa ikiendelea kuwa mbaya”,alisema Kukongwa.
 
Kwa upande wake Afisa tarafa ya Kasanga Peter Mankambila amesema kwa kawaida ugali wa muhogo huliwa maara baada ya kurowekwa kwa zaidi ya siku tatu inaonyesha familia hiyo ilikula ugali huo bila ya kuroweka vizuri.
 
“Muhogo unaolimwa kwenye maeneo haya ya Mwambao wa Ziwa Tanganyikahuwa ni mchungu kupita kiasi, hivyo bila kuuloweka vizuri ni lazima ukuletee madhara kiafya kama ilivyotokea kwa familia hii”,alieleza.
 
Nae Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa Geoge Simba Kyando alisema kuna taarifa mchanganyiko juu ya tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa zaidi mara baada ya uchunguzi.
 
“Kuna taarifa tofauti kwenye tukio hili, kwani inadaiwa kuwa familia hiyo ilitumia dawa ya kienyeji na zingine zinadai kuwa walitumia ugali wa muhogo hivyo tunashindwa kupata taarifa sahihi ni zipi, tutatoa taarifa zaidi uchunguzi ukikamilika na kubaini chanzo halisi cha vifo vya watu hao’’,alisema kamanda Kyando.
chanzo: zanzibar24.

Comments