Mamia ya wananchi wamejitokeza katika viwanja vya Mwembeyanga katika maadhimisho ya siku ya watu duniani na kupata huduma ya afya ya uzazi wa mpango, kupima Virusi vya Ukimwi na ushauri nasaha bure.
Naibu Waziri wa Afya, Hamis Kigwangala alitarajiwa kuhudhuria katika maadhimisho hayo lakini aliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Otilia Gowele.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni ‘Uzazi wa mpango huwezesha watu na kuendeleza mataifa.’
Dk Gowele amesema wakati tukihimiza uchumi wa viwanda, nchi inahitaji rasilimali watu wenye ujuzi na uwezo wa kushindana na hao ni matunda ya uzazi wa mpango kwa kuwa wanakuwa wamehudumiwa vizuri.
"Tulipofikia hapa hatuhitaji huduma za afya, elimu na miundombinu bali tunahitaji huduma zilizo bora, haya yatawezekana endapo taifa litapunguza ongezeko la idadi ya watu. Tunaongezeka kwa kasi, mwaka 1961 tulikuwa Milioni tisa lakini mpaka mwaka 2012 tulikuwa zaidi ya million 45," amesema Dk Gowele.
chanzo:Mwananchi.
Comments