Upinzani katika tanuru la moto.

Wanasiasa wa upinzani kukamatwakamatwa, kufunguliwa kesi, kuwekwa mahabusu kwa saa 48 kwa amri ya wakuu wa wilaya, madiwani kujiuzulu, mikutano ya ndani kuingiliwa, na baadhi ya viongozi wao kuteuliwa kushika nyadhifa serikalini ni mojawapo ya mambo ambayo vyama vya siasa vinapitia kwa sasa.
Mbali na hayo, kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara, migogoro ya uongozi ambayo hatima yake inategemea vyombo vya Serikali na wabunge kuadhibiwa mara kwa mara, ni masuala mengine yanayoviweka vyama hivyo katika hali ngumu pengine kuliko wakati mwingine wowote tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani nchini mwaka 1992.

Vyama vinavyopitia katika hali hiyo ni Chadema, ambacho kinaongoza upinzani nchini, CUF, ambayo ni chama kikuu cha upinzani Zanzibar na ACT Wazalendo, ambacho pamoja na upya wake, kinaonekana kuendelea kujijenga.
Hali hiyo inajenga maswali kama vyama vya upinzani vitaweza kustahimili misukosuko hiyo katika kipindi hiki ambacho ni cha maandalizi ya kujijenga kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu mwaka mmoja baadaye.
Maswali na hofu inayoibuka kutokana na hali hiyo ni  pamoja na iwapo upinzani utadhoofu na hata kufa kabisa lakini wengine wameenda mbali na kusema misukosuko hiyo inawatengenezea msingi imara wa kujiimarisha.
Baadhi ya wachambuzi wa duru za kisiasa wamesema matukio yanayoendelea yanaweza kuwaongezea umaarufu kupitia huruma ya wananchi (political sympathies).
Misukosuko mingine dhidi ya wapinzani ni zuio la mikutano ya hadhara na katika baadhi ya maeneo hata ile ya ndani.
Pia, kuna wimbi la wanachama na viongozi wa upinzani kuhamia CCM, kuzuiliwa kwa ‘Bunge live’ ambalo lilikuwa ni jukwaa pana kujiongezea umaafuru na mitaji pamoja na utendaji wa Rais John Magufuli unaoonekana kukusanya mitaji kadhaa ya kisiasa ikiwamo sakata la makinikia, dawa za kulevya, watumishi hewa, vyeti feki, utumbuaji majipu na kadhalika.
Lakini wakati kukiwa na dhana hiyo ya kudhoofisha upinzani, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole anakanusha vikali tuhuma hizo.
Polepole alimwambia mwandishi wa gazeti hili hivi karibuni kwamba vyama vya upinzani vinapaswa kutathmini udhaifu wa demokrasia yake na si kuihusisha CCM pale vinapopata matatizo.
Chama kinachopitia katika hali ngumu zaidi ni CUF, ambayo inapambana na mwenyekiti wake, Profesa Ibrahimu Lipumba. Mgogoro huo ulianza baada ya Lipumba kuandika barua ya kujiuzulu Agosti mwaka 2015 na kutaka kurejea madarakani mwaka mmoja baadaye, akidai CUF haikupitisha uamuzi wake wa kujiondoa madarakani.
Baadaye Mkutano Mkuu uliidhinisha uamuzi wake wa kujiuzulu, lakini Profesa Lipumba hakukubaliana nao na tangu wakati huo amekuwa na mgogoro na chama chake. Msimamo wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kumtambua, ndio unazidi kukiweka pabaya chama hicho kutokana na upande unaomuunga mkono katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa na msimamo mkali.
Mgogoro huo uko mahakamani, huku Profesa Lipumba akizidi kujijenga kutokana na mamlaka za Serikali, kutambua shughuli zake baada ya Wakala wa Usajili na Ufilisi (Nida) kutambua bodi ya wadhamini iliyoteuliwa na Lipumba.
Wakati CUF ikihaha kutatua mgogoro wake, zuio la mikutano ya hadhara limeathiri shughuli za kujitangaza za vyama vya upinzani, kama Chadema ilivyonufaika na operesheni tofauti kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopita.
Hivi karibuni, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa alihojiwa polisi kwa madai ya kutoa kauli za uchochezi.
Siku tano zilizopita, viongozi na wanachama 51 wa Chadema walikamatwa wakiwa kwenye kikao cha ndani wilayani Chato. Viongozi hao ni sehemu ya viongozi kadhaa ambao wamekuwa wakikamatwa, kuachiwa au wakati mwingine kufunguliwa kesi na wengine kuhukumiwa kwenda jela.
Pia, Agosti mwaka jana, viongozi zaidi ya 60 wakiwamo wabunge na viongozi wa kitaifa  walikamatwa na Jeshi la Polisi likiongozwa na OCD wa Oysterbay wakiwa katika kikao cha ndani cha Kamati Kuu kilichokuwa kikifanya katika Hoteli ya Giraffe.
Machi mwaka huu,  mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema aliachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu baada ya kukaa ndani kwa miezi minne.
 Wakati vyama hivyo vikishindwa kujitanua, ACT-Wazalendo imejikuta ikipoteza vigogo wake wawili walioteuliwa kushika nafasi za juu serikalini.
 Aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho, 2015, Anna Mghwira ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, wakati aliyekuwa mshauri, Profesa Kitila Mkumbo ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maji.
Ushahidi wa kudhoofika kwa upinzani nchini unadhihirishwa na matokeo ya utafiti wa Twaweza uliofanyika kati ya Machi 31 na Aprili 17 mwaka huu, yakionyesha asilimia 63 ya waliohojiwa walisema wako karibu zaidi na CCM huku asilimia 17 wakiwa karibu na Chadema, asilimia moja (ACT), asilimia moja (CUF) na asilimia moja kwa NCCR Mageuzi.
 Wachambuzi wa masuala ya kisiasa walioulizwa na gazeti hili kuhusu matukio hayo, walisema  huenda yakaviongezea nguvu vyama vya upinzani au kuvidhoofisha.
Profesa Gaudence Mpangalla wa Chuo Kikuu cha Ruaha, alisema changamoto hizo zinazojitokeza kwa upinzani zinaviongezea nguvu na ushawishi zaidi kwa wananchi.
Alisema kwa sasa wananchi wameelimika na hupima haki na misingi ya demokrasia.
“Kwa hiyo ninaamini kuwabana wapinzani kwa kutumia nguvu hiyo ni kuwaongezea nguvu, mfano mzuri utakumbuka walivyojitokeza kuunga mkono upinzani kwenye uchaguzi wa 2015, licha ya vikwazo, kashfa kwa wagombea upinzani lakini wananchi hawakujali, kwa hiyo kila tukio wananchi wanalipima,” alisema.
Profesa huyo wa sayansi ya siasa na utawala bora, alisema hofu ya matokeo ya uchaguzi wa 2015, ndiyo imechangia kujitokeza kwa mazingira hayo baada ya CCM kufanya tathmini na utafiti wa kushuka kwa umaarufu wake katika uchaguzi huo.
“Sasa sijui kama waliona njia sahihi ni kudhoofisha? Mimi ninaamini si njia sahihi. CCM ingeachia uhuru kwa kuwa  ndiyo tafsiri ya mfumo wa vyama vingi. Kwa mazingira haya hatuwezi kuwashindanisha wakati mmoja anafanya siasa mwingine amezuiwa,” alisema.
Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar, Profesa Abdul Sherrif alisema kujijenga au kudhoofika kwa upinzani ikuategemeana na hali ya matukio na uvumilivu huku akionyesha hofu ya kudhoofika zaidi kupitia mgogoro wa CUF.
“Kwa mpasuko wa CUF, kura za wanachama zitasambaa na itakuwa furaha kwa chama kilichopo madarakani (CCM), wengine watakata tamaa na wengine wanaweza kujiunga na vyama vingine kwa hasira baada ya kuona haki haitendeki. Muhimu ni kuchukua tahadhari kwa njia zinazotumika,” alisema Profesa Sherrif.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Richard Mbunda alitoa mtazamo na njia za kuua upinzani bila kutumia nguvu hiyo inayotumika kwa sasa.
 Mbunda alisema kabla ya mfumo wa vyama vingi, chama tawala kilikuwa na upinzani wa ndani ya chama tu na siyo nje hivyo kiliweza kuwashughulikia wanachama wake ikiwamo kuwafukuza, huku akitolea mfano kutimuliwa kwa Maalim Seif.
“Lakini kwa mfumo wa vyama vingi sasa, njia pekee ya kudhoofisha upinzani ni kujitangaza na kazi inayofanywa na Rais, kukamata mafisadi, kuwajibisha watumishi na kurejesha nidhamu. Ni mambo yanayotosha kuua upinzani kwa sababu amewapokonya ajenda zao,” alisema.
“Upinzani ungekuwa na wakati mgumu sana kwa utawala huu endapo angewaacha huru, wasingekuwa na ajenda yoyote ingefika wakati wangempongeza lakini kwa sasa inabidi watumie ‘political sympathies’ kama mtaji wao kwa wananchi, wakilalamika wananchi wanawaonea huruma na inawajenga.”
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema pamoja na kutafuta mbinu mpya za kuendesha siasa, kamwe hawarudi katika siasa za chama kimoja.
Lissu alitoa kauli hiyo mwaka jana alipokutana na wanafunzi wa Programu ya Election Bridge Academy inayoendeshwa na taasisi ya Afrika Kusini iitwayo KAS Media. “Lakini kama wamebana je, tutarudi nyuma na kuomba Mungu atusaidie? Ni lazima kupambana zaidi, ni lazima kupaza sauti na mataifa mengine yajue Tanzania kuna nini kinaendelea,” alisema.
chanzo:Mwananchi.

Comments