Serikali ina mpango wa kupeleka pendekezo bungeni litakaloipa mamlaka ya kusimamia fukwe zote katika ukanda wa Bahari ya Hindi nchini kutoka mikononi mwa watu ili kukuza utalii na kuongeza mapato.
Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika kuwa zaidi ya asilimia 95 ya fukwe kuanzia mkoani Tanga hadi Mtwara zinamilikiwa na watu binafsi wasiozitumia kitalii, jambo lililoifanya Serikali kushindwa kuwekeza kwenye fukwe hizo.
Akizungumza jana wakati wa uchambuzi wa ripoti ya ‘Maendeleo ya Kiuchumi Afrika ya mwaka 2017:
Mabadiliko na Ukuaji Shirikishi katika Sekta ya Utalii’ itakayozinduliwa leo ulimwenguni kote, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Aloyce Nzuki amesema Serikali ina mpango wa kupanua wigo wa utalii kwenye fukwe hizo.
“Bahati mbaya hao wanaomiliki fukwe hizo hawazitumii kitalii, kwa hiyo tutapeleka andiko bungeni ili Serikali isimamie fukwe hizo kwa madhumuni ya kitalii,” amesema Dk Nzuki na kusisitiza kuwa tayari serikali imezitambua fukwe hizo.
Akichambua ripoti hiyo, Mtaalamu Mwelekezi wa Taasisi ya MRA, Onesmo Kenneth amesema ripoti hiyo imebainisha changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na miundombinu hafifu ya barabara kuelekea kwenye maeneo ya hifadhi.
Kenneth amesema ripoti hiyo inasisitiza pia ushiriki wa wananchi katika sekta ya utalii kwa sababu ina fursa nyingi ambazo zinatoa ajira kwao na serikali kuongeza mapato yake kwenye Pato la Taifa.
chanzo:mwananchi.
Comments