Majaliwa, Samia wamuaga karani wa Baraza la Mawaziri.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameungana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, viongozi waandamizi wa Serikali na wananchi kuuaga mwili wa aliyekuwa karani wa Baraza la Mawaziri, Hassan Shebuge.
Mwili wa Shebuge umeagwa leo (Julai 7) nyumbani kwake Mbagala Majimatitu jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu imesema maziko yanatarajiwa kufanyika kesho (Julai 8) katika Kijiji cha Funta wilayani Bumbuli, Mkoa wa Tanga.

Shebuge alifariki dunia jana (Julai 6) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupatwa na shinikizo la damu.
Kwa niaba ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Majaliwa amesema kifo hicho ni pigo kwa Serikali.
Amesema Shebuge alikuwa mpole na mwadilifu, aliyetoa mchango mkubwa kufanikisha uamuzi na utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa ufanisi.
 “Wajibu wetu sote ni kumuombea kwa Mwenyezi Mungu,” amesema.
Katibu Mkuu Ikulu, Alphayo Kidata akisoma wasifu wa Shebuge amesema alizaliwa Mei 25, 1969 wilayani Korogwe, Tanga.
Alipata elimu ya msingi katika shule ya Mkwakwani kuanzia mwaka 1977 hadi 1983 na alipata elimu ya sekondari katika shule ya Usagara kuanzia 1984 hadi 1987. Shule zote ziko mkoani Tanga.
Kidata amesema mwaka 1988, alijiunga na Shule ya Sekondari ya Ilboru mkoani Arusha kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na cha sita.
Amesema mwaka 1992 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupata Shahada ya Sanaa na Ustawi wa Jamii mwaka 1995 na mwaka 1998 alipata Shahada ya Uzamili ya Sanaa na Ustawi wa Jamii. Pia, alipata mafunzo mengine ndani na nje ya nchi.
chanzo:Mwananchi.

Comments