Korea
Kaskazini imeendelea na mpango wake wa majaribio ya silaha nzito ambapo
jana usiku imeripotiwa kufyatua kombora lingine zito kutoka Magharibi
mwa eneo lake.
Kwa
mujibu wa taarifa zilizotolewa na maafisa wa Japan na Korea Kaskazini,
kombora hilo lilifyatuliwa majira ya saa tatu na dakika arobaini usiku
kwa saa za eneo hilo, na lilitua katika eneo muhimu la kiuchumi la
bahari nchini Japan.
Shirika
la habari la Yonhap limekariri tamko la jeshi la Japan kuwa kombora
lililofyatuliwa lilisafiri umbali wa kilometa 930 na lilichukua dakika
40 kabla ya kutua, kitendo kilichozua taharuki.
Hili
ni jaribio la 11 la makombora ya Korea Kaskazini kwa mwaka huu, ingawa
majaribio ya hivi karibuni yanaonekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Jaribio la mwisho lilikuwa mwezi Mei mwaka huu, katika maeneo mawili tofauti ambayo yote yalielekezwa baharini nchini Japan.
Katibu
Mkuu wa Baraza la Mawazili la Japan, Yoshihide Suga ameeleza kuwa
uchokozi unaofanywa na Korea Kaskazini hauvumiliki. Ameongeza kuwa taifa
hilo linalaani kwa nguvu zote vitendo hivyo na hatua stahiki
zitachukuliwa.
Naye
Rais wa Korea Kusini, Moon Jae ametoa wito wa kufanyika kwa kikao cha
dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili hatua za
Korea Kaskazini, wito aliousisitiza pia wakati wa kikao chake na Rais wa
Marekani, Donald Trump ndani ya Ikulu ya Marekani.
Rais Trump pia aliendelea na mfululizo wa maonyo kwa Korea Kaskazini, akisema kuwa uvumilivu umefika kikomo na sasa ‘inatosha’.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments