
Zitto ametumia ukurasa wake wa Facebook kuandika yafuatayo:
Hili la Mkurugenzi Mkuu wa EWURA linahusu tangazo la leseni ya Kampuni ya kifisadi ya IPTL?
Ni muhimu sana Rais afahamu kwamba kuna kazi kubwa ya chinichini
inafanywa na wasaidizi wake ( sina hakika kama yeye Rais anajua na au
ameruhusu kazi hiyo ) kuendeleza wizi huu wa watu wa PAP ya Harbinder
Singh Seth na IPTL. Kwenye kesi ya Standard Chartered Bank dhidi ya
TANESCO huko mahakama ya ICSID ambapo TANESCO wanatakiwa kulipa shilingi
352 bilioni kwa Benki hiyo, Wanasheria wa TANESCO na wale wa PAP/IPTL
wanashirikiana kwa karibu mno.
Kwenye rufaa, TANESCO wametakiwa waweke
fedha hizo kwanza kwenye akaunti ya Benki ya nje kabla ya rufaa
kusikilizwa.
PAP/IPTL wanalinda ufisadi wao kwa kujifanya wanashirikiana na TANESCO kwenye kesi. Kwenye Taarifa ya PAC kuhusu Tegeta Escrow Account, tuliweka wazi kuwa PAP/IPTL waliweka dhamana kuwa ikitokea madai yeyote yale dhidi ya TANESCO basi PAP/IPTL italipa. Madai yametokea, matapeli hawa wanajifanya kushirikiana na Shirika letu na Wanasheria wa Serikali wanawasaidia matapeli hawa na sasa wanataka kuwaongezea leseni ya Biashara.
Kwanini Serikali isitumie ile Indemnity kuwataka PAP kulipa
hizi fedha? Kwanini Serikali inayosema inapambana na ufisadi
inawakumbatia mafisadi wa PAP/IPTL? Kwanini Serikali iliyoonyesha
ujasiri wa kupambana na Kampuni kubwa kama Acacia/Barrick inayumbishwa
na matapeli hawa? Tena tapeli mmoja tu Harbinder Singh Seth?
Vyombo vya Serikali pia vinahusika na kuwalinda hawa matapeli. Kwa
mfano, huko ICSID Shirika letu la TANESCO kupitia wanasheria wake
wamepeleka hoja kwamba Maazimio ya Bunge kuhusu Tegeta Escrow hayana
msingi wowote wa kisheria na kwamba Bunge linapiga porojo tu.
Wanasheria
hawa wameomba Ofisi ya Bunge iwape barua kuthibitisha kuwa Maamuzi ya
bunge hayana msingi wowote na ni maoni tu yanaweza kudharauliwa na
kutupiliwa mbali. Shirika la Umma linalosimamiwa na Bunge linapeleka
barua kwenye vyombo vya kibeberu kuwa Bunge porojo tupu.
Pia kwa kudanganywa na PAP/IPTL, TANESCO wamepeleka madai kuwa PAC
ilihongwa kufikia maamuzi yaliyofikiwa na Bunge.
Wametengeneza barua
pepe za kujaribu kushawishi madai yao hayo na hata Taasisi muhimu kama
PCCB waliingia kwenye mkenge huo na kuniita kunihoji.
Niliwapa
ushirikiano wote na kuwapa simu na computer zangu wachunguze barua pepe
zile za kuchonga wakakuta hakuna lolote. Sikuwaacha, niliwaambia kuwa
wao ni mawakala wa mashetani.
Wanashirikiana na matapeli kuwaibia
Watanzania. Idara ya Usalama wa Taifa, inahusika moja kwa moja na kazi
hii inayofanywa na PAP/IPTL ili kufanikisha mradi huu wa kitapeli. Sina
hakika kama Rais aliidhinisha haya maana TISS na PCCB wanawajibika kwa
Rais moja kwa moja.
Hivyo, inawezekana kabisa mpango wa kuongeza leseni ya IPTL
akawajibishwa mtu wa EWURA kwa sababu ndiye alitoa tangazo la leseni,
lakini huyo mtu wa EWURA anaweza kuwa ameshinikizwa na watu wa Usalama
wa Taifa kufanya hivyo.
Mimi naamini Rais, kwa jinsi alivyo, hawezi kuwa
anahusika na haya matapeli, lakini Rais mtumbuaji anakaaje miezi 20
kwenye Kiti za Enzi bila kumaliza suala la IPTL ilhali kuna Maazimio ya
Bunge yanayopaswa kutekelezwa?
Nawapa kazi ndogo Watanzania, tazameni lile Tangazo la EWURA kuhusu
IPTL nililowawekea hapa siku limetoka. Tazameni umiliki na wamiliki wa
IPTL hivi sasa.
Kuna hisa 16% kwa kampuni mbili zenye majina ya ujanja
ujanja. Kina nani hao wamegawiwa hizo hisa tena wakati wa Uongozi wa
Rais John Pombe Magufuli.
chanzo: zanzibar24.
Comments