Waziri
wa Mambo ya Nje wa Norway Mhe. Borge Brende amemhakikishia Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa
Norway itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na
Tanzania hususani kuboresha huduma za kijamii na uwekezaji katika miradi
mikubwa ya maendeleo.
Mhe.
Borge Brende aliyeongozana na Balozi wa Norway hapa nchini Mhe.
Hanne-Marie Kaarstad amesema hayo leo tarehe 30 Juni, 2017 Ikulu Jijini
Dar es Salaam muda mfupi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mhe.
Rais Magufuli.
Mhe.
Borge Brende amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa
anazozifanya katika kupambana na rushwa, kukabiliana na matumizi mabaya
ya ofisi za umma na kusimamia vizuri uchumi na shughuli za maendeleo na
kwamba Norway inavutiwa na juhudi hizo na ipo tayari kushirikiana na
Serikali ya Awamu ya Tano kuimarisha zaidi juhudi hizo.
“Uhusiano
wa Tanzania na Norway umedumu kwa miaka 55 na tumeshirikiana katika
mambo mengi yakiwemo kuendeleza elimu na miundombinu mbalimbali na sasa
tunatarajia kushirikiana zaidi na Tanzania kwa kuwekeza katika miradi
mikubwa kama vile uzalishaji wa umeme, kuchakata gesi na kuzalisha
mbolea” amesema Mhe. Borge Brende.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Norway kwa
mchango wake mkubwa ilioutoa kwa Tanzania tangu uhusiano na ushirikiano
kati ya nchi hizi uanze na amesema Serikali ya Awamu ya Tano
inakaribisha ushirikiano zaidi na Norway hasa uwekezaji utakaokuwa na
manufaa kwa pande zote mbili.
“Hivi
sasa tumedhamiria kujenga mradi wa kuzalishaji umeme kwa kutumia
maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), lakini pia nchi yetu ina
vyanzo vingine vya kuzalisha umeme kama vile maporomoko ya maji katika
mito mingine, gesi ambayo mpaka sasa tumegundua futi za ujazo zaidi ya
Trilioni 57, tuna makaa ya mawe, jua na upepo mwingi kwa ajili ya
kuzalisha umeme, kwa hiyo tunawakaribisha wawekezaji kutoka Norway
tushirikiane kuwekeza kwenye maeneo hayo” Amesema Mhe. Rais Magufuli.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments