Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, amewatuhumu viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa wanayapa silaha baadhi ya makundi ya wanamgambo wa nchi hiyo.
Zeid Ra'ad Al Hussein, sambamba na kuashiria ripoti zinazoonyesha kuwa baadhi ya viongozi wa nchi hiyo wamekuwa wakiyapa silaha baadhi ya makundi ya waasi yanayofanya uhalifu nchini humo amesema kuwa, hivi karibuni makundi hayo yalitekeleza mashambulizi ya kutisha dhidi ya raia wa kawaida katika mji wa Kasaï, katikati mwa nchi.
Hadi sasa mapigano yaliyoanza tangu miezi minane iliyopita kati ya askari wa usalama wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wanamgambo wa kikabila katika mji huo, yamesababisha zaidi ya watu 3000 kuuawa, ingawa serikali ya Kinshasa inataja idadi ndogo ya wahanga hao.
Ni muda sasa ambapo maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hususan mkoa wa Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yamekuwa yakishuhudia machafuko yanayosababishwa na uepo wa wanamgambo wa waasi.
Tofauti za kikabila, kikaumu na kiuchumi ni sababu kuu zinazochangia kuwepo makundi ya wanamgambo na waasi katika maeneo hayo. Mikoa ya mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina utajiri mkubwa wa madini ya almasi na dhahabu ambapo jumla ya asilimia 65 ya maeneo yenye utajiri huo, yako chini ya udhibiti wa wanamgambo na askari wa jeshi la serikali. Kwa kuzingatia utajiri huo, weledi wengi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, baadhi ya nchi zimekuwa zikihusika katika kuyaunga mkono makundi ya waasi kwa lengo la kupora maliasili za nchi hiyo.
Kwa mujibu wa weledi hao, madola ya Magharibi yanahesabiwa kuwa wahusika wakuu wa kuchochea machafuko na mapigano katika nchi za Afrika hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kwa njia hiyo sambamba na kuhalalisha uwepo wao, yaweze kupora utajiri wa nchi hizo.
Ufisadi wa baadhi ya viongozi wa na kadhalika hatua yao ya kuendelea kuzikumbatia nchi za Magharibi, ni sababu nyingine inayotoa mwanya kwa uungaji mkono wa nyuma ya pazia wa madola hayo kwa makundi ya wanamgambo.
Itakumbukwa kuwa, baada ya waasi wa Kihutu kutekeleza mauaji hayo ya kimbari nchini Rwanda, walikimbilia nchini Kongo DR.
Hii ni katika hali ambayo baadhi ya Watutsi walioweza kuokoka katika mashambulizi ya Wahutu hao huko Rwanda, walikimbilia pia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuunda safu mpya ya kimapambano dhidi ya Wahutu wenye misimamo mikali. Ni miaka kadhaa sasa ambapo mapigano hayo ya Wahutu dhidi ya Watutsi nchini Kongo DR yamesababisha mauaji ya watu wengi nchini humo.
Ni kwa ajili hiyo ndio maana baadhi ya nchi za Kiafrika zikiwemo Rwanda na Uganda zikatuhumiwa kwa uungaji mkono kwa makundi ya waasi yanayotekeleza jinai dhidi ya binaadamu.
Hii ni katika hali ambayo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amewatuhumu baadhi ya viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi kwa kuhusika na uungaji mkono wa makundi ya wanamgambo, huku nchi hiyo ikiwa na zaidi ya askari elfu 17 wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo uepo wa askari hao haujaweza kuzuia machafauko nchini humo. Matatizo ya wakimbizi, kuenea kwa maradhi na kukosekana kwa chakula na madawa, yote hayo yanasababishwa na kuendelea kwa mapigano hususan katika maeneo ya kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.
chanzo:parstoday.
Comments