SMZ yazuia suluhu kesi za ubakaji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed AboudSERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imewataka wazazi kuacha mara moja mtindo wa kusuluhisha kesi za udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo za ubakaji kwa njia ya kienyeji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema muswada wa marekebisho ya sheria ya makosa ya jinai unaotazamiwa kuwasilishwa mbele ya Baraza la Wawakilishi utawabana watu wanaofanya suluhu kwa kesi za udhalilishaji wa kijinsia.
 

Alisema kitendo cha jamii kuleta suluhu katika kesi za udhalilishaji wa kijinsia kwa kiasi kikubwa kimechangia kuzorota kwa kesi hizo na wahusika kuwatia hatiani.

Alisema katika marekebisho ya sheria ya mwenendo wa kesi za jinai, suala la kuleta suluhu katika kesi hizo halikubaliki kwa sababu tayari kesi za ubakaji ni kosa la jinai. 

Akifafanua, alisema jamii imekuwa na malalamiko mengi kwamba kesi za udhalilishaji wa kijinsia zinakwama katika ngazi za upelelezi katika Jeshi la Polisi na mahakamani. 

Lakini uchunguzi zaidi umebaini kwamba kesi hizo licha ya kuchukua muda mrefu katika ngazi ya upelelezi katika jeshi la Polisi lakini jamii imekuwa na tabia ya kuleta suluhu na kukubaliana na watu waliofanya matukio hayo.

Alisema ni jambo baya zaidi wakati mwingine kesi ya ubakaji inayomkabili mwanamke, wazazi hukubaliana kwa kuleta suluhu ya kiasi kidogo cha fedha. 

Aidha katika marekebisho ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, suala la dhamana kwa watuhumiwa wa makosa ya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji watanyimwa dhamana. 

Alisema moja ya malalamiko makubwa ya jamii kuhusu mwenendo wa kesi za udhalilishaji wa kijinsia, ni kwa watuhumiwa wa makosa ya aina hiyo kupewa dhamana na Jeshi la Polisi na baadaye kuonekana wakizurura mitaani na kutishia kuvuruga ushahidi ikiwemo kutoa vitisho.
chanzo:Habarileo.

Comments