Kubaki dunia mtazamaji wa maafa yanayoifika Yemen chini ya kivuli cha uungaji mkono wa Marekani kwa Saudia.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura ameonya kuwa Yemen inakaribia kusambaratika kikamilifu, na kwamba wananchi wake wanakabiliwa na vita vya umwagaji damu vilivyoanzishwa na Saudi Arabia sambamba na baa la njaa na mripuko wa ugonjwa thakili wa kipindupindu huku dunia ikibaki kuwa mtazamaji tu.
Stephen O'Brien, alitoa indhari hiyo wakati akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa wakati sasa umefika wa kuhitimisha janga kubwa zaidi duniani la mahitaji ya dharura ya chakula na kuiwezesha nchi ya Yemen kuwa na uhai tena.
Yemen inakabiliwa na hali mbaya zaidi ya kibinadamu; na hivi sasa inaelekea kusambaratika kikamilifu kutokana na kuendelea kuteketea kwa moto wa vita uliowashwa na Saudi Arabia kwa msaada wa kijeshi wa Marekani.
Misaada na uungaji mkono wa aina mbalimbali unaotolewa na wale wanaojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu kwa muungano vamizi unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen umeigeuza nchi hiyo eneo la maonyesho ya jinai dhidi ya binadamu, jinai za kivita na hali mbaya ya usalama wa chakula.
Kubomolewa na kuteketezwa miundombinu ya Yemen vikiwemo vituo vya tiba na afya na kuzingirwa kutokea angani, nchi kavu na baharini kumeifanya nchi hiyo ikabiliwe na janga la kiafya na maafa makubwa ya kibinadamu. Kuenea maradhi thakili ya kipindupindu, ni kielelezo cha wazi cha kukosekana mazingira ya kiafya nchini Yemen.
Kwa mujibu wa ripoti za taasisi zinazohusika na masuala ya afya, tangu mwishoni mwa mwezi Aprili hadi sasa, zaidi ya watu 500 wamefariki dunia kwa kipindupindu na wengine 55,206 wameambukizwa ugonjwa huo theluthi moja kati yao wakiwa ni watoto wadogo. Inakadiriwa kuwa hadi miezi sita ijayo, watu wengine laki moja na nusu watakuwa wamekumbwa na ugonjwa huo hatari.
Hali hii ni dhihirisho la upeo wa juu wa upuuzaji wa kutochukua hatua unaofanywa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na mgogoro na hali mbaya zaidi ya kibinadamu inayoshuhudiwa duniani.
Kukiri Mkuu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwamba Yemen inaelekea kusambaratika kikamilifu ni ishara ya kukatishwa tamaa na utendaji wa Baraza la Usalama kuhusiana na utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo; baraza ambalo baadhi ya wanachama wake wa kudumu ni washirika wa jinai zinazofanywa na utawala wa Aal Saud dhidi ya wananchi madhulumu wa Yemen kutokana na kuuzia utawala huo silaha za kisasa zikiwemo hata zilizopigwa marufuku unazozitumia dhidi ya wananchi hao.
Utumizi wa mabomu ya Kimarekani yaliyopigwa marufuku ya vishada unaofanywa na Saudia katika mashambulio yake ya anga unachangia moja kwa moja machungu na mateso wanayoendelea kupata hivi sasa wananchi wa Yemen.
Hali hiyo inaonyesha jinsi wale wanaojinasibu kuwa watetezi wa haki za binadamu wanavyozitoa kafara haki hizo kupitia mashirikiano yao ya kiuchumi na utawala wa Aal Saud.
Kusainiwa mkataba wa kijeshi wa dola bilioni 110 kati ya Saudia na Marekani kulikofuatiwa na mdundiko wa ngoma ya kuzungusha panga hewani uliochezwa na Donald Trump na Mfalme Salman kulikuwa sawa na kulidhihaki suala la msingi la haki za binadamu; kwani tangu mwezi Machi mwaka 2015 hadi sasa wananchi wa Yemen wanauliwa kwa halaiki katika mashambulio ya kinyama yanayofanywa na Saudia na kutokana na ukosefu wa chakula na huduma za afya; na leo hii kwa mujibu wa Mkuu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Yemen yenyewe iko kwenye ukingo wa lindi la usambaratikaji kamili..
chanzo:parstoday.
Comments