Askari wa Umoja wa Mataifa washindwa kurejesha amani CAR.


Licha ya kupita miaka minne tokea kutumwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, lakini bado nchi hiyo inashuhudia machafuko ambayo yamepelekea mamia ya watu kuuawa.


Kwa mujibu wa toleo la leo Alkhamisi la gazeti la Le Monde la nchini Ufaransa, licha ya kutumwa askari hao nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2013 kwa lengo la kulinda amani na kurudisha utulivu nchini humo lakini bado asilimia 20 ya raia wa nchi hiyo wameikimbia nchi hiyo kutokana na machafuko yanayochochewa na wanamgambo.

Gazeti hilo limeandika kuwa watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wakiwemo maafisa wa serikali na viongozi wa Kikristo na Kiislamu wanawakosoa askari hao kwa kushindwa kurudisha amani na utulivu nchini humo.
Lengo kuu la kutumwa askari wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo ya Kiafrika lilikuwa ni kuzuia kuenea machafuko na kulinda raia wa nchi hiyo dhidi ya mashambulio ya wanamgambo lakini sasa ukosoaji dhidi ya kikosi hicho umeongezeka na hasa kufuatia mauaji ya kinyama yaliyotekelezwa mapema mwezi Mei uliopita katika mji wa Bangassou, kusini mashariki mwa nchi.

chanzo;parstoday.

Comments