Watoto milioni 1.4 wanakabiliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu Somalia.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetahadharisha kuwa huenda watoto milioni 1.4 wa Somalia wakapoteza maisha kutokana na utapiamlo wa kiwango cha juu.

Marixie Mercado, Msemaji wa UNICEF amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa, kufikia mwishoni mwa mwaka huu, idadi ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo itaongezeka na kufikia milioni 1.4, kiwango ambacho ni sawa na ongezeko la asilimia 50 ukilinganisha na mwaka jana 2016.


Amesema watoto laki mbili na 75 elfu miongoni mwao wapo katika hali mbaya zaidi, na yumkini wakapoteza maisha karibuni hivi iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa.

Mercado ameongeza kuwa, watoto wenye utapiamlo wa kiwango cha juu wapo katika hatari ya kupoteza maisha mara tisa kutokana na kipindupindu, kuharisha na surua.
 
Somalia ambayo imekuwa kwenye vita vya ndani na hususan mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab kwa zaidi ya miongo miwili, kwa sasa inasumbuliwa na ukame mkubwa unaoandamana na njaa. 
 
Kwa mujibu wa Mpango wa Chakula Duniani WFP, watu laki mbili na 60 elfu waliaga dunia kutokana na baa la njaa lililosababishwa na ukame kama wa sasa katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika mwaka 2011, huku nusu ya vifo hivyo vikiwakabili watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano. 
chanzo:parstoday.

Comments