Shahidi akwamisha kesi ya Scorpion.

Kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi inayomkabili Salum Njetwe maarufu ‘’Scorpion’’  imeshindwa kuendelea kusikilizwa baada ya upande wa mashtaka  kudai shahidi ambaye walimtegemea kuendelea kuulizwa maswali na wakili anayemtetea Scorpion, kuwa  bado ni mgonjwa.
Kesi hiyo iliyopo katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imeshindwa kuendelea kutoka na shahidi namba nane katika kesi hiyo, Deus Magosa (45) maarufu kama Pamba D, kushindwa kufika mahakama hapo kutokana na kuugua ugonjwa wa Kisukari na Shinikizo la damu.

Magosa ambaye ni kamanda wa ulinzi Shirikishi mmiliki wa meza za Pool  table katika eneo la Buguruni,  alitakiwa  kuulizwa maswali na wakili Juma Nassoro anayemtetea mshtakiwa Scorpion.
Hii ni mara ya pili kwa kesi hiyo kuahirishwa, ambapo April 18, mwaka huu kesi hiyo iliahirishwa baada ya shahidi huyo kuwa mgonjwa na kushindwa kufika mahakamani.
Scorpion amepanda kizimbani leo (Jumanne) katika Mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji.
Wakili wa Serikali Chesensia Gavyole amedai kuwa kutokana na kupokea taarifa ya mgonjwa huyo kutoka hospitalini kwamba anaendelea na matibabu aliomba tarehe nyingine ya kutajwa na kumleta shahidi mwingine kuendelea.
Kutokana na ombi hilo, hakimu Flora alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 15, mwaka huu na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 6, mwaka jana eneo la Buguruni Sheli wilayani Ilala.
 chanzo:mwananchi.

Comments