
Mpango huo utakwenda sambamba na uimarishaji wa Miundombinu ya
uingiaji Nchini inayojumuisha Bandari, Viwanja vya Ndege , barabara za
ndani , Nishati pamoja na Tafiti zitakazosaidia kutoa maamuzi katika
mipango hiyo ya Maendeleo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo
wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi
ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika Kikao cha Bajeti cha Baraza
la Wawakilishi Zanzibar kilichoanza leo katika Majengo ya Baraza hilo
yaliopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema Serikali itaendelea kuweka mkazo katika
kugharamia uendeshaji wake na kutoa huduma bora kwa Wananchi kwa
kutumia rasilmali zilizopo kwa umakini mkubwa na kuhakikisha matumizi
yote yanaleta tija kwa Umma.
Alisema utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2020 ikiwa katika
kipindi cha mwisho cha miaka mitano unaenda sambamba na uidhinishwaji
wa awamu ya Tatu ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini {
MKUZA 111}.
Balozi Seif alieleza kwamba hiyo inamaanisha wazi kwamba Malengo ya
Taifa bado yanadhamiria utekelezaji wa Mipango hiyo Mikuu ambayo
imekusudia kukuza Uchumi, kuimarisha huduma za Jamii pamoja na
kuimarisha Demokrasia na Utawala Bora.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwamba hali ya ukuaji wa
uchumi wa Nchi imepelekea kuongezeka kwa Pato la Taifa kwa mwaka 2016
ambalo limeongezeka na kufikia thamani ya Shilingi 2,309.5 Bilioni
ikilinganishwa na thamani ya shilingi 1,633.0 Bilioni Mwaka 2015.

Akigusia mvua za masika zinazoendelea kunyesha hapa Nchini na kuleta
athari kubwa kwa Wananchi walio wengi Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif aliwatahadharisha Wananchi kuendelea kuchukua
tahadhari za kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo miripuko
ya maradhi yanayosababishwa na uchafuzi wa maji.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inawasisitiza Wananchi
kuepuka kujenga katika maeneo hatarishi ambayo mazingira yake yanaweza
kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa hasa wakati wa mvua kubwa
zinazonyesha kama mabondeni, kwenye njia za asili za maji na pembezoni
mwa milima hasa Kisiwani Pemba.
Balozi Seif alitoa wito kwa wananchi kuendelea kufuata maelekezo
yanayotolewa na wataalamu wa afya juu ya usafi wa mazingira ikiwemo
kunawa mikono mara watokapo kujisaidia na kabla ya kula.
Kwa upande wa wafanyabiashara Balozi Seif aliwakumbusha kuendelea
kufuata masharti yaliyowekwa juu ya biashara zao kwa kuzingatia suala la
usafi na ulinzi wa afya za Wananchi ili kujikinga na maradhi ya
mripuko.
Akigusia janga a dawa za kulevya linaloendelea kuiathiri jamii Nchini
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali
yaMapinduzi ya Zanzibar kupitia Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti
wa Dawa za Kulevya imetoa mafunzo kwa wadau katika shehia zenye Banadari
Rasmi na zisizo Rasmi.
Alisema hatua hiyo ililenga kuweka wazi mbinu mbali mbali
zinazotumiwa na wahalifu katika kupitishia dawa za kulevya ambapo
washiriki wa mafunzo hayo wapatao 186 walitoa kwenye Shehia zipatazo 94
zenye Bandari hizo.
Balozi Seif alisema Kamati ya Kitaalamu ya Tume hiyo iliweza kupanga
mikakati ya udhibiti wa dawa za kulevya, uimarishaji wa kinga dhidi ya
matumizi ya dawa hizo pamoja na kuzisaidia Nyumba za upataji nafuu kwa
vijana walioathirika na dawa za kulevya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizipongeza Nchi Rafiki, Taasisi,
Makampuni na washirika wa maendeleo ndani na nje ya Nchi waliojitolea
kuunga mkono harakati za Maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar na kupiga
hatua kubwa Kiuchumi na ustawi wa Jamii.
Balozi Seif alisema michango ya washirika na Mataifa hayo marafiki
imewezesha kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa huduma bora
za Kijamii na kuleta maendeleo katika Taifa zima.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliliomba Baraza la Wawakilishi
liidhinishe jumla ya shilingi Bilioni 44,837,577,000/- kwa Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Taasisi zake kwa ajili ya
kutekeleza Programu zake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
10/5/2017.
chanzo: zanzibar24.
Comments